Ebr 10

Ebr 10

Kafara ya Kristo Inatosha

1Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.[#Ebr 8:5; 7:19]

2Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi?

3Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka.[#Law 16:21]

4Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

5Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema,[#Zab 40:6-8]

Dhabihu na toleo hukutaka,

Lakini mwili uliniwekea tayari;

6Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;

7Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa)

Niyafanye mapenzi yako, Mungu.

8Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati),

9ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili.

10Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.[#Ebr 9:12,28]

11Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi.[#Kut 29:38]

12Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu;[#Zab 110:1]

13tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake.

14Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.

15Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema,

16Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana,[#Yer 31:33; Ebr 8:10]

Nitatia sheria zangu mioyoni mwao,

Na katika nia zao nitaziandika;

ndipo anenapo,

17Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa.[#Yer 31:34; Ebr 8:12]

18Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.

Wito wa kuwa Wavumilivu

19Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu,[#Mt 27:51]

20njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake;[#Ebr 9:8]

21na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;[#Zek 6:11; Hes 12:7]

22na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi.[#Law 8:30; Eze 36:25; Efe 5:26]

23Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu;[#Ebr 4:14]

24tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri;[#Ebr 13:1]

25wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.[#Ebr 3:13]

26Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;[#Ebr 6:4-8; 1 Tim 2:4]

27bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.[#Isa 26:11]

28Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.[#Kum 17:6; 19:15; Hes 15:30; 35:30]

29Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?[#Kut 24:8; Ebr 2:3]

30Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.[#Kum 32:35-36; Zab 135:14; Rum 12:19]

31Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.[#Ebr 12:29]

32Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu;[#Ebr 6:4]

33pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo.[#1 Kor 4:9]

34Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo.[#Mt 6:20; 19:21,29]

35Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu.[#Ebr 11:6]

36Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.[#Ebr 6:12; Lk 21:19]

37Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana,[#Hab 2:3-4; Isa 26:20; Lk 21:28; Yak 5:8]

Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.

38Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani;[#Rum 1:17; Gal 3:11]

Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.

39Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania