The chat will start when you send the first message.
1Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni,[#Zab 110:1; Ebr 4:14]
2mhudumu wa patakatifu, na wa ile hema ya kweli, ambayo Bwana aliiweka wala si mwanadamu.
3Maana kila kuhani mkuu huwekwa ili atoe vipawa na dhabihu; kwa hiyo lazima huyu naye awe na kitu cha kutoa.
4Kama angekuwa juu ya nchi, asingekuwa kuhani; maana wako watoao sadaka kama iagizavyo sheria;
5watumikiao mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni, kama Musa alivyoagizwa na Mungu, alipokuwa tayari kuifanya ile hema; maana asema, Angalia ukavifanye vitu vyote kwa mfano ule ulioonyeshwa katika mlima.[#Kut 25:40; Kol 2:17]
6Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora.[#Ebr 7:22; 12:24; 2 Kor 3:6]
7Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili.
8Maana, awalaumupo, asema[#Yer 31:31-34; Ebr 10:16,17]
Angalia, siku zinakuja, asema Bwana,
Nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya;
9Halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao,[#Kut 19:5,6]
Katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri.
Kwa sababu hawakudumu katika agano langu,
Mimi nami sikuwajali asema Bwana.
10Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli
Baada ya siku zile, asema Bwana;
Nitawapa sheria zangu katika nia zao,
Na katika mioyo yao nitaziandika;
Nami nitakuwa Mungu kwao,
Nao watakuwa watu wangu.
11Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake,
Na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana;
Kwa maana wote watanijua,
Tangu mdogo wao hata mkubwa wao.
12Kwa sababu nitawasamehe maovu yao,
Na dhambi zao sitazikumbuka tena.
13Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu. Lakini kitu kianzacho kuwa kikuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.[#Rum 10:4]