Hos 6

Hos 6

Mwito wa Toba

1Njoni, tumrudie BWANA; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu.[#Ayu 5:18; Kut 15:26; Isa 30:26; Yer 30:17; Eze 34:16]

2Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake.

3Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua BWANA; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi.[#Mit 2:1-9; Mt 13:11; Ayu 29:23]

Uovu wa Israeli na Yuda

4Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema.

5Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga.[#Yer 1:10; Ebr 4:12]

6Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.[#Mit 21:3; Zab 50:8; Yn 17:3; Mt 9:13; 12:7]

7Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana.

8Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu.

9Na kama vile makundi ya wanyang’anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana.

10Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi.

11Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu.[#Zab 126:1]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania