The chat will start when you send the first message.
1Ole wao wawekao amri zisizo za haki, na waandishi waandikao maneno ya ushupavu;
2ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya maskini wa watu wangu haki yao; ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao!
3Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa, na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je! Mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtauacha wapi?[#Hos 9:7; Lk 19:44]
4Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini yao waliouawa. Pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.
5Ole wake Ashuru! Fimbo ya hasira yangu, ambaye gongo lililo mkononi mwake ni ghadhabu yangu![#Isa 14:24-27; Nah 1:1—3:19; Sef 2:13-15]
6Nitamtuma juu ya taifa lenye kukufuru, nitampa maagizo juu ya watu wa ghadhabu yangu, ateke nyara, na kuchukua mateka, na kuwakanyaga kama matope ya njiani.
7Lakini hivyo sivyo akusudiavyo mwenyewe, wala sivyo moyo wake uwazavyo; maana katika moyo wake akusudia kuharibu, na kukatilia mbali mataifa, wala si mataifa machache.[#Mik 4:12]
8Maana asema, Je! Wakuu wangu si wote wafalme?[#2 Fal 18:24]
9Je! Kalno si kama Karkemishi? Hamathi si kama Arpadi? Samaria si kama Dameski?[#Amo 6:2; 2 Nya 35:20; Yer 46:2; Hes 13:21; 2 Sam 8:9; 2 Fal 23:33; Isa 10:9; 2 Fal 16:9]
10Kama vile mkono wangu ulivyofikilia falme za sanamu, ambazo sanamu zao za kuchongwa zilikuwa bora kuliko sanamu za Yerusalemu na za Samaria;
11je! Sitautenda Yerusalemu na sanamu zake vile vile kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?
12Basi, itakuwa, Bwana atakapokuwa ameitimiza kazi yake yote juu ya mlima Sayuni na juu ya Yerusalemu, nitayaadhibu matunda ya kiburi cha moyo wake mfalme wa Ashuru, na majivuno ya macho yake.
13Kwa maana amesema, Kwa nguvu za mkono wangu nimetenda jambo hili, na kwa hekima yangu; maana mimi nina busara; nami nimeiondoa mipaka ya watu, nikaziteka akiba zao, nikawaangusha waketio juu ya viti vya enzi kama afanyavyo shujaa.[#Kut 15:9; Zab 20:7; Isa 37:24]
14Na mkono wangu umezitoa mali za mataifa kama katika kioto cha ndege; na kama vile watu wakusanyavyo mayai yaliyoachwa, ndivyo nilivyokusanya dunia yote; wala hapana aliyetikisa bawa, wala kufumbua kinywa, wala kulia.
15Je! Shoka lijisifu juu yake alitumiaye? Je! Msumeno ujitukuze juu yake auvutaye? Ingekuwa kana kwamba bakora ingewatikisa waiinuao, au fimbo ingemwinua yeye ambaye si mti.[#Yer 51:20; Rum 9:20,21]
16Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, atawapelekea kukonda watu wake walionona; na badala ya utukufu wake kutawashwa kuteketea kama kuteketea kwa moto.
17Na mwanga wa Israeli utakuwa ni moto, na Mtakatifu wake atakuwa mwali wa moto; nao utateketeza na kula mbigili zake na miiba yake katika siku moja.
18Naye atauteketeza utukufu wa msitu wake, na wa shamba lake linalositawi, tangu nafsi hata nyama ya mwili, itakuwa kama vile afapo mtu aliye mgonjwa.
19Na miti ya msitu wake itakayosalia itakuwa michache, hata mtoto ataweza kuihesabu.
20Tena itakuwa katika siku hiyo mabaki ya Israeli, na hao waliopona wa nyumba ya Yakobo, hawatamtegemea tena yeye aliyewapiga, bali watamtegemea BWANA, Mtakatifu wa Israeli, kwa kweli.
21Mabaki, nao ni mabaki ya Yakobo, watamrudia Mungu, aliye mwenye nguvu.
22Maana watu wako, Ee Israeli, wajapokuwa wengi kama mchanga wa pwani, ni mabaki tu watakaorudi; kuangamiza kumekusudiwa, kunakofurika kwa haki.[#Mik 5:3; Rum 9:27]
23Kwa maana Bwana, BWANA wa majeshi, atayatimiza maangamizo yaliyokusudiwa katika nchi yote.[#Isa 28:22; Dan 9:27]
24Kwa hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Enyi watu wangu mkaao katika Sayuni, msiogope Ashuru, ingawa akupiga kwa fimbo, na kuliinua gongo lake juu yako, kwa namna ya Kimisri.
25Maana bado kitambo kidogo tu ghadhabu itakoma, na hasira yangu itageukia kuwaangamiza.[#Dan 11:36]
26Na BWANA wa majeshi ataamsha mjeledi juu yake, kama vile alivyopiga Midiani karibu na jabali la Orebu; na fimbo yake itakuwa juu ya bahari, naye ataiinua kwa namna ya Kimisri.
27Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.[#Zab 105:15]
28Amefika Ayathi; amepita kati ya Migroni; ameweka mizigo yake huko Mikmashi;[#Neh 11:31]
29wamevuka kivuko; wamekwenda kulala katika Geba; Rama unatetemeka; Gibea wa Sauli umekimbia.[#1 Sam 13:23]
30Piga kelele sana, Ee binti Galimu; sikiliza, Ee Laisha; ole wako, maskini Anathothi![#1 Sam 25:44]
31Madmena ni mkimbizi; wenyeji wa Gebimu wamejikusanya wakimbie;[#Yos 15:31]
32siku hii ya leo atasimama huko Nobu; anatikisa mkono wake juu ya mlima wa binti Sayuni, mlima wa Yerusalemu.[#1 Sam 21:1]
33Angalia, Bwana, BWANA wa majeshi, atayakata matawi kwa nguvu za kutisha; nao walio warefu wa kimo watakatwa; na hao walioinuka wataangushwa chini;
34naye atavikata vichaka vya msitu kwa chuma; na Lebanoni utaanguka kwa mkono wake aliye mwenye uweza.