Isa 20

Isa 20

Isaya Aigiza Kushindwa kwa Misri na Kushi

1Katika mwaka ule jemadari yule alipofika Ashdodi, alipotumwa na Sargoni mfalme wa Ashuru; naye alipigana na Ashdodi akautwaa;[#2 Fal 18:17; #20:1 hapa, kwa Kiebrania ni Tartan.]

2wakati huo BWANA alinena kwa kinywa cha Isaya, mwana wa Amozi, akisema, Haya, uvue nguo ya magunia viunoni mwako, na viatu vyako miguuni mwako.[#Zek 13:4; 1 Sam 19:24]

3Naye akafanya hivyo akaenda uchi, miguu yake haina viatu. BWANA akasema, Kama vile mtumishi wangu Isaya anavyokwenda uchi, hana viatu, awe ishara na ajabu kwa muda wa miaka mitatu juu ya Misri na juu ya Kushi;[#Isa 8:18]

4vivyo hivyo mfalme wa Ashuru atawachukua uchi, wafungwa wa Misri, na watu wa Kushi waliohamishwa, watoto kwa wazee, hawana viatu, matako yao wazi, Misri iaibishwe.[#2 Sam 10:4; Mik 1:11]

5Nao watafadhaika, na kuona haya kwa ajili ya Kushi, matumaini yao, na Misri, utukufu wao.[#2 Fal 18:21; Isa 31:1-3]

6Na mwenyeji wa nchi ya pwani atasema katika siku hiyo, Angalia, haya ndiyo yaliyowapata watu wale tuliowatumaini, ambao tuliwakimbilia watuokoe na mfalme wa Ashuru; na sisi je! Twawezaje kupona?

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania