Yn 1

Yn 1

Neno akawa Mwili

1Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.[#1 Yoh 1:1,2; Yn 17:5; Ufu 19:13]

2Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.[#Mit 8:22]

3Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.[#Kol 1:16,17; Ebr 1:2]

4Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu.[#Yn 5:26]

5Nayo nuru yang’aa gizani, wala giza halikuiweza.[#Yn 3:19]

6Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohana.[#Mt 3:1; Mk 1:4; Lk 3:1-2; 1:13-17,57-80]

7Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye.[#Lk 3:3]

8Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru.[#Yn 1:20]

9Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu.

10Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua.[#Yn 1:3-5]

11Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea.

12Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;[#Gal 3:26]

13waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.[#Yn 3:5,6]

14Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.[#Isa 7:14; 2 Pet 1:16,17; Isa 60:1; Lk 9:32]

15Yohana alimshuhudia, akapaza sauti yake akasema, Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Ajaye nyuma yangu amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.[#Yn 1:27,30; Mt 3:11]

16Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema.[#Yn 3:34; Kol 1:19]

17Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo.[#Rum 6:14; 10:4; Kut 34:6; Zab 25:10; 40:10; 85:10]

18Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua.[#Yn 6:46; 1 Yoh 4:12; Mt 11:27; Lk 10:22; 1 Tim 6:16]

Ushuhuda wa Yohana Mbatizaji

19Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani?[#Lk 3:15,16]

20Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo.[#Mdo 13:25]

21Wakamwuliza, Ni nini basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La.[#Kum 18:15,18; Mal 4:5; Mt 17:10; Yn 6:14; 7:40]

22Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako?

23Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya.[#Isa 40:3; Mt 3:3; Mk 1:3; Lk 3:4]

24Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo.

25Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule?[#Mt 21:25]

26Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi.[#Mt 3:11; Mk 1:7,8]

27Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake.[#Yn 3:26; Mdo 13:25]

28Hayo yalifanyika huko Bethania ng’ambo ya Yordani, alikokuwako Yohana akibatiza.[#Mt 3:6,13]

Mwanakondoo wa Mungu

29Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu![#Yn 1:36; Isa 53:7]

30Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu.[#Yn 15:27]

31Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji.

32Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake.[#Mt 3:16; Mk 1:10; Lk 3:22]

33Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu.[#Lk 3:2; Mt 3:16]

34Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.[#Mt 3:17]

Wanafunzi wa kwanza wa Yesu

35Tena siku ya pili yake Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake.

36Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu![#Yn 1:29; Isa 53:7]

37Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu.

38Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?

39Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi.

40Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata Yesu.[#Mt 4:18-22]

41Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo).[#1 Sam 2:10; Zab 2:2]

42Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).[#Mt 16:18; Mk 3:16]

Yesu Awaita Filipo na Nathanaeli

43Siku ya pili yake alitaka kuondoka kwenda Galilaya, naye akamwona Filipo. Yesu akamwambia, Nifuate.[#Mt 8:22; Mk 2:14]

44Naye Filipo alikuwa mtu wa Bethsaida, mwenyeji wa mji wa Andrea na Petro.

45Filipo akamwona Nathanaeli, akamwambia, Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.[#Kum 18:18; Isa 7:14; 53:2; Yer 23:5; Eze 34:23]

46Nathanaeli akamwambia, Laweza neno jema kutoka Nazareti? Filipo akamwambia, Njoo uone.[#Yn 7:41,52]

47Basi Yesu akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake.[#Zab 32:2; 73:1; Mwa 25:27]

48Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.

49Nathanaeli akamjibu, Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.[#2 Sam 7:14; Yn 6:69; Zab 2:7; Mt 14:33; 16:16]

50Yesu akajibu, akamwambia, Kwa sababu nilikuambia, Nilikuona chini ya mtini, waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya.

51Akamwambia, Amin, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.[#Mwa 28:12; Mt 4:11; Mk 1:13]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania