Yn 14

Yn 14

Yesu ni Njia ya kwenda kwa Baba

1Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi.[#Yn 14:27; Mk 11:22]

2Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.

3Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.[#Yn 12:26; 17:24]

4Nami niendako mwaijua njia.

5Tomaso akamwambia, Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?

6Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.[#Ebr 10:20; Mt 11:27; Yn 11:25; Rum 5:1,2]

7Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba; tangu sasa mnamjua, tena mmemwona.

8Filipo akamwambia, Bwana, utuonyeshe Baba, yatutosha.

9Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?[#Yn 12:45; Ebr 1:3; Mt 17:17]

10Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake.[#Yn 12:49]

11Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! Hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe.[#Yn 14:20; Yn 10:25,38]

12Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba.[#Mk 16:19,20]

13Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.[#Yn 15:7; Mk 11:24; 1 Yoh 5:14]

14Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.[#Yn 16:23,24]

Ahadi ya kupewa Roho Mtakatifu

15Mkinipenda, mtazishika amri zangu.[#Yn 15:10; 1 Yoh 5:3]

16Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;[#Yn 14:26; 15:26; 16:7; 1 Yoh 2:1]

17ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.[#Yn 7:39; 16:13; Mt 10:20; Rum 8:26]

18Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.

19Bado kitambo kidogo na ulimwengu haunioni tena; bali ninyi mnaniona. Na kwa sababu mimi ni hai, ninyi nanyi mtakuwa hai.[#Yn 16:16]

20Siku ile ninyi mtatambua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.[#Yn 17:21-23]

21Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.[#2 Kor 3:18; 1 Yoh 5:3]

22Yuda (siye Iskariote), akamwambia, Bwana, imekuwaje ya kwamba wataka kujidhihirisha kwetu, wala si kwa ulimwengu?[#Mdo 10:41]

23Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.[#Yn 13:34; 14:21; Mit 8:17; Mt 18:20; 28:20; Efe 3:17; 2 Kor 6:16]

24Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka.[#Yn 7:16; 1 Yoh 2:5]

25Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu.

26Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.[#Yn 14:16; Mt 10:19]

27Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga.[#Yn 1:16,33; Flp 4:7]

28Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi.[#Yn 14:3,6,18; Lk 24:52]

29Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.[#Yn 13:19]

30Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.[#Yn 12:31; Efe 2:2]

31Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.[#Yn 10:18; Mt 26:46; Mk 14:42]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania