Yn 15

Yn 15

Yesu ni Mzabibu wa Kweli

1Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.[#Yer 2:21; Zab 80:8]

2Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa.[#Mt 15:13]

3Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia.

4Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.

5Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote.[#1 Kor 12:12,27; 2 Kor 3:5]

6Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.[#Mt 3:10; 13:40]

7Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.[#Mk 11:24]

8Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.[#Mt 5:16]

9Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu.

10Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.[#Yn 8:29; 14:15; 1 Yoh 2:4,8]

11Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.[#Yn 17:13]

12Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi.[#Yn 13:34; 15:17; 1 Yoh 3:11,23; 2 Yoh 1:5; Mk 12:30]

13Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.[#Yn 10:12; 1 Yoh 3:16]

14Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.[#Yn 8:31; Mt 12:50; 28:20]

15Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.

16Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni.[#Yn 6:70; 13:18]

17Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.

Chuki ya Ulimwengu

18Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.[#Yn 7:7; 1 Yoh 3:13]

19Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.[#1 Yoh 4:5; Yn 17:14; Lk 6:22]

20Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.[#Mt 10:24; Lk 6:40; Yn 13:16]

21Lakini haya yote watawatenda kwa ajili ya jina langu, kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.[#Yn 10:22; 16:3; Mt 5:11; Mk 13:13]

22Kama nisingalikuja na kusema nao, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa hawana udhuru kwa dhambi yao.

23Yeye anichukiaye mimi humchukia na Baba yangu.[#Yn 5:23; 1 Yoh 2:23; Lk 10:16]

24Kama nisingalitenda kwao kazi asizozitenda mtu mwingine, wasingalikuwa na dhambi; lakini sasa wametuona mimi na Baba yangu, na kutuchukia.[#Yn 14:11]

25Lakini litimie lile neno lililoandikwa katika torati yao, Walinichukia bure.[#Zab 35:19; 69:4]

26Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia.[#Yn 14:26; Lk 24:49]

27Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.[#Lk 1:2; Mdo 1:8; 5:32]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania