The chat will start when you send the first message.
1Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe;[#Yn 11:14; 13:1]
2kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele.[#Mt 11:27]
3Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma.[#1 Yoh 5:20; 1 The 1:9]
4Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye.[#Yn 4:34]
5Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako.[#Yn 1:1; 17:24; Flp 2:6]
6Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika.[#Yn 17:9; Mt 6:9]
7Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako.
8Kwa kuwa maneno uliyonipa nimewapa wao; nao wakayapokea, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, wakasadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.[#Yn 16:30]
9Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;[#Yn 6:37,44]
10na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; nami nimetukuzwa ndani yao.[#Yn 16:15; Lk 15:31]
11Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.[#Yn 10:30; Mt 6:13]
12Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie.[#Zab 41:9; 109:8; Yn 13:18; 6:39; 2 The 2:3]
13Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao.[#Yn 15:11]
14Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.[#Yn 15:19]
15Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu.[#2 The 3:3; 1 Yoh 5:18; Mt 6:13; Lk 22:32]
16Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.
17Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli.[#Yn 6:63]
18Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni.[#Yn 20:21]
19Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli.[#Ebr 10:10]
20Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.[#Yn 17:9]
21Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.[#Gal 3:28]
22Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja.[#Mdo 4:32]
23Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.[#1 Kor 6:17; Gal 2:20]
24Baba, hao ulionipa nataka wawe pamoja nami po pote nilipo, wapate na kuutazama utukufu wangu ulionipa; kwa maana ulinipenda kabla ya kuwekwa msingi ulimwengu.[#Yn 10:29; 12:26; Efe 1:4]
25Baba mwenye haki, ulimwengu haukukujua; lakini mimi nalikujua, na hao wamejua ya kuwa ndiwe uliyenituma.
26Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao.