Yn 18

Yn 18

Kusalitiwa na Kukamatwa kwa Yesu

1Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng’ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake.[#Mt 26:36; Mk 14:32; Lk 22:39; 2 Sam 15:23]

2Naye Yuda, yule aliyetaka kumsaliti, alipajua mahali pale; kwa sababu Yesu alikuwa akienda huko mara nyingi pamoja na wanafunzi wake.[#Mt 26:47-56; Mk 14:43-52; Lk 22:47-53; #Lk 21:37]

3Basi Yuda, akiisha kupokea kikosi cha askari na watumishi waliotoka kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo, akaenda huko na taa na mienge na silaha.

4Basi Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawaambia, Ni nani mnayemtafuta?[#Yn 19:28]

5Wao wakamjibu, Ni Yesu Mnazareti. Yesu akawaambia, Ni mimi. Yuda naye aliyemsaliti alikuwa amesimama pamoja nao.

6Basi alipowaambia, Ni mimi, walirudi nyuma, wakaanguka chini.

7Basi akawauliza tena, Mnamtafuta nani? Wakasema, Yesu Mnazareti.

8Yesu akajibu, Nimekwisha kuwaambieni ya kwamba ni mimi; basi ikiwa mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao.

9Ili litimizwe lile neno alilolisema, Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja wao.[#Yn 17:12]

10Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko.

11Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?[#Mt 26:39; Mk 14:36; Lk 22:42]

Yesu mbele ya Kuhani Mkuu

12Basi wale askari na yule jemadari na wale watumishi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga.[#Mt 26:57-75; Mk 14:53-72; Lk 22:54-71]

13Wakamchukua kwa Anasi kwanza; maana alikuwa mkwewe Kayafa, yule aliyekuwa Kuhani Mkuu mwaka ule.

14Naye Kayafa ndiye yule aliyewapa Wayahudi lile shauri ya kwamba yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya watu.[#Yn 11:49-50]

Petro Amkana Yesu

15Wakamfuata Yesu, Petro na mwanafunzi mwingine. Na mwanafunzi huyo alikuwa amejulikana na Kuhani Mkuu, akaingia pamoja na Yesu katika behewa ya Kuhani Mkuu.[#Yn 20:3; 21:20; Mdo 3:1]

16Lakini Petro akasimama nje mlangoni. Basi yule mwanafunzi mwingine aliyejulikana na Kuhani Mkuu akatoka, akasema na mngoja mlango, akamleta Petro ndani.

17Basi yule kijakazi, aliyekuwa mngoja mlango, akamwambia Petro, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi mmojawapo wa mtu huyu? Naye akasema, Si mimi.

18Na wale watumwa na watumishi walikuwa wakisimama, wamefanya moto wa makaa; maana ilikuwa baridi; wakawa wakikota moto. Petro naye alikuwapo pamoja nao, anakota moto.

Kuhani Mkuu Amhoji Yesu

19Basi Kuhani Mkuu akamwuliza Yesu habari za wanafunzi wake, na habari za mafundisho yake.

20Yesu akamjibu, Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi; sikuzote nalifundisha katika sinagogi na katika hekalu, wakusanyikapo Wayahudi wote; wala kwa siri mimi sikusema neno lo lote.[#Yn 7:14,26; Mt 10:27]

21Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia ni nini niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.

22Basi aliposema hayo, mtumishi mmojawapo aliyesimama karibu alimpiga Yesu kofi akisema, Wamjibu hivi Kuhani Mkuu?[#Yn 19:3; Mdo 23:2]

23Yesu akamjibu, Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?

24Basi Anasi akampeleka hali amefungwa kwa Kayafa, Kuhani Mkuu.

Petro Amkana tena Yesu

25Na Simoni Petro alikuwa akisimama huko, anakota moto. Basi wakamwambia, Wewe nawe, je! Hu mwanafunzi wake mmojawapo? Naye akakana, akasema, Si mimi.

26Mtumwa mmojawapo wa Kuhani Mkuu, naye ni jamaa yake yule aliyekatwa sikio na Petro, akasema, Je! Mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?

27Basi Petro akakana tena, na mara akawika jimbi.

28Kisha wakamchukua Yesu kutoka kwa Kayafa mpaka Praitorio, nayo ikawa alfajiri; lakini wao wenyewe hawakuingia ndani ya ile Praitorio, wasije wakanajisika, bali wapate kuila Pasaka.[#Mt 27:2,11-30; Mk 15:1-19; Lk 23:1-25; #18:28 maana ni Nyumba ya Uliwali.]

29Basi Pilato akawatokea nje, akasema, Ni mashitaka gani mnayoleta juu ya mtu huyu?

30Wakajibu, wakamwambia, Kama huyu asingekuwa mtenda mabaya, tusingemleta kwako.

31Basi Pilato akawaambia, Haya! Mtwaeni ninyi, mkamhukumu kwa ile torati yenu! Wayahudi wakamwambia, Sisi hatuna ruhusa ya kuua mtu.[#Yn 19:6,7; Mdo 18:15]

32Ili litimie lile neno lake Yesu alilolisema, akionyesha ni mauti gani atakayokufa.[#Yn 3:14; 12:32; 19:32,33; Mt 20:19]

33Basi Pilato akaingia tena ndani ya Praitorio, akamwita Yesu, akamwambia, Je! Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?

34Yesu akamjibu, Wewe wasema hivi kwa nafsi yako, au watu wengine walikuambia habari zangu?[#Mt 16:13]

35Pilato akajibu, Ama! Ni Myahudi mimi! Taifa lako na wakuu wa makuhani ndio waliokuleta kwangu. Umefanya nini?[#Yn 1:11; Mt 21:39]

36Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.

37Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na kwa ajili ya haya mimi nalikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.[#1 Tim 6:13; Yn 8:47; 10:27]

38Pilato akamwambia, Kweli ni nini?

Yesu Ahukumiwa Kifo

Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake.

39Lakini kwenu kuna desturi ya mimi kuwafungulia mtu mmoja wakati wa Pasaka; basi, mwapenda niwafungulie Mfalme wa Wayahudi?

40Basi wakapiga kelele tena kusema, Si huyu, bali Baraba. Naye yule Baraba alikuwa mnyang’anyi. i.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania