Ayu 14

Ayu 14

1Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke[#Ayu 15:14; Zab 51:5; Mhu 2:23]

Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu.

2Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa;[#Isa 40:6; Yak 1:10; 1 Pet 1:24]

Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe.

3Nawe, je! Wafumbua macho yako kumwangalia mtu kama yeye,[#Zab 144:3; 143:2]

Na kunitia katika hukumu pamoja nawe?

4Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana awezaye.[#Mwa 5:3; Zab 51:5; Yn 3:5; Rum 5:12; Efe 2:3]

5Kwa kuwa siku zake zimeamriwa, hesabu ya miezi yake unayo wewe,

Nawe umemwekea mipaka yake asiyoweza kuipita;

6Acha kumwangalia yeye, apate kupumzika,[#Zab 39:13]

Hata atakapoitimiza siku yake, kama aliyeajiriwa.

7Kwani yako matumaini ya mti, ya kuwa ukikatwa utachipuka tena,

Wala machipukizi yake hayatakoma.

8Ijapokuwa mizizi yake huchakaa mchangani,

Na shina lake kufa katika udongo;

9Lakini kwa harufu ya maji utachipuka,

Na kutoa matawi kama mche.

10Lakini mwanadamu hufa, huifariki dunia;

Naam, mwanadamu hutoa roho, naye yupo wapi?

11Kama vile maji kupwa katika bahari,

Na mto kupunguka na kukatika;

12Ni vivyo mwanadamu hulala chini, asiinuke;[#Zab 102:26; Isa 51:6; Mdo 3:21; Rum 8:20; 2 Pet 3:7; Ufu 20:14]

Hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka,

Wala kuamshwa usingizini.

13Laiti ungenificha kuzimuni,

Ukanilinda kwa siri, hata ghadhabu zako zitakapopita,

Na kuniandikia muda ulioamriwa, na kunikumbuka!

14Mtu akifa, je! Atakuwa hai tena?[#Ayu 13:15; Zab 16:10; 1 Kor 15:42-58; Flp 3:21]

Mimi ningengoja siku zote za vita vyangu,

Hata kufunguliwa kwangu kunifikilie.

15Wewe ungeita, nami ningekujibu;[#Ayu 13:22; Zab 50:4; Yn 5:28; 1 The 4:16]

Ungekuwa na tamaa ya kazi ya mikono yako.

16Lakini sasa wazihesabu hatua zangu;[#Kum 32:34; Ayu 10:6,14; 13:27; Zab 56:8; Mit 5:21; Yer 32:19; Hos 13:12]

Je! Huchungulii dhambi yangu?

17Kosa langu limetiwa muhuri mfukoni,

Nawe waufunga uovu wangu.

18Lakini, tazama, mlima ukianguka hutoweka,

Nalo jabali huondolewa mahali pake;

19Maji mengi huyapunguza mawe;

Mafuriko yake huuchukua mchanga wa nchi;

Nawe matumaini ya wanadamu wayaangamiza.

20Wewe wamshinda nguvu sikuzote, naye hupita aende zake

Wabadili sura zake, na kumpeleka aondoke.

21Wanawe hufikilia heshima, wala yeye hajui;[#1 Sam 4:20; Zab 39:6; Mhu 9:5; Isa 63:16]

Kisha wao huaibishwa, lakini yeye hana habari zao.

22Lakini mwili ulio juu yake una maumivu,[#Zab 49:14; Mit 14:32; Mt 8:12]

Na nafsi yake ndani huomboleza.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania