The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Bildadi, Mshuhi, akajibu, na kusema,
2Je! Hata lini utayategea maneno mitambo?
Fikiri, kisha baadaye tutanena.
3Twahesabiwa kuwa wanyama kwa sababu gani,[#Ayu 12:7; Zab 73:22]
Tena kuwa wanajisi machoni pako?
4Wewe ujiraruaye mwenyewe katika hasira yako,[#Ayu 13:14]
Je! Dunia itaachwa kwa ajili yako wewe?
Au jabali litaondolewa mahali pake?
5Naam, mwanga wa waovu utazimika,[#Ayu 21:17; Mit 13:9]
Wala mwali wa moto wake hautang’aa.
6Mwanga hemani mwake utakuwa giza,
Nayo taa iliyo juu yake itazimishwa.
7Hatua zake za nguvu zitasongwa,
Na shauri lake mwenyewe litamwangusha chini.
8Kwani ametupwa katika wavu na miguu yake mwenyewe,
Naye huenda juu ya matanzi.
9Tanzi litamshika kisigino chake,
Na mtambo utamgwia.
10Amefichiwa tanzi chini,
Na mtego amewekewa njiani.
11Matisho yatamtia hofu pande zote,[#Ayu 6:4; Zab 73:19; Yer 6:25; 2 Kor 5:11]
Na kumfukuza karibu na visigino vyake.
12Nguvu zake zitaliwa na njaa,[#Ayu 15:23; 1 The 5:3]
Na msiba utakuwa tayari kwa kusita kwake.
13Utakula via vya mwili wake,
Naam, mzaliwa wa kwanza wa mauti atavila via vyake.
14Atang’olewa katika hema yake aliyokuwa akiitumaini;[#Ayu 8:14; Zab 112:10; Mit 10:28; Mt 7:26,27]
Naye atapelekwa kwake mfalme wa utisho.
15Ambacho si chake kitakaa katika hema yake;[#Mwa 19:24]
Kiberiti kitamwagwa juu ya makazi yake.
16Chini, mizizi yake itakaushwa;
Na juu, tawi lake litasinyaa.
17Kumbukumbu lake litakoma katika nchi,[#Zab 34:16; Mit 2:22]
Wala hatakuwa na jina mashambani.
18Atakimbizwa kutoka mwangani hata gizani,
Na kufukuzwa atoke duniani.
19Hatakuwa na mwana wala mjukuu kati ya watu wake,[#Isa 14:22; Yer 22:30]
Wala hatasalia mtu hapo alipokaa.
20Hao wanaokaa magharibi watastaajabia siku yake,
Kama vile wanaokaa mashariki walivyotiwa hofu.
21Hakika ndivyo yalivyo makazi ya wapotovu,[#Yer 9:3; 1 The 4:5; 2 The 1:8; Tit 1:16]
Na hapa ni mahali pake asiyemjua Mungu.