Ayu 29

Ayu 29

Ayubu Amalizia Hoja Zake

1Kisha Ayubu akaendelea na mithali yake, na kusema,

2Laiti ningekuwa kama nilivyokuwa katika miezi ya kale,

Kama katika siku hizo Mungu aliponilinda;

3Hapo taa yake ilipomulika juu yangu kichwani,[#Ayu 18:6; Zab 18:28]

Nami nilitembea gizani kwa njia ya mwanga wake;

4Kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa,[#Zab 25:14; Mit 3:32]

Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu;

5Wakati Mwenyezi alipokuwa akali pamoja nami,

Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka;

6Wakati hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi,[#Mwa 49:11; Kum 32:13; Zab 81:16]

Nalo jabali liliponimiminia mito ya mafuta!

7Wakati nilipotoka kwenda mjini, hata langoni,

Nilipokitengeza kiti changu katika njia kuu,

8Hao vijana waliniona wakajificha,

Nao wazee wakaniondokea na kusimama;

9Wakuu wakanyamaa wasinene,

Na kuweka mikono yao vinywani mwao;

10Sauti yao masheki ilinyamaa,[#Zab 137:6]

Na ndimi zao zilishikamana na makaakaa yao.

11Maana sikio liliponisikia, ndipo likanibarikia;

Na jicho liliponiona, likanishuhudia.

12Kwa sababu nalimwokoa maskini aliyenililia;[#Zab 72:12; Mit 21:13]

Yatima naye, na yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia.

13Baraka yake yeye aliyekuwa karibu na kupotea ilinijia;

Nikaufanya moyo wa mjane kuimba kwa furaha.

14Nalijivika haki, ikanifunika,[#Zab 132:9; Rum 13:14; Efe 6:14]

Adili yangu ilikuwa kama joho na kilemba.

15Nalikuwa macho kwa kipofu,[#Hes 10:31]

Nalikuwa miguu kwa aliyechechemea.

16Nalikuwa baba kwa mhitaji,[#Mit 29:7]

Na daawa ya mtu nisiyemjua naliichunguza.

17Nami nilizivunja taya za wasio haki,

Na kumpokonya mawindo katika meno yake.

18Ndipo niliposema, Nitakufa ndani ya kioto changu,[#Zab 30:6]

Nami nitaziongeza siku zangu kama mchanga;

19Shina langu limeenea hata kufika majini,[#Zab 1:3; Yer 17:8]

Na umande hukaa usiku kucha katika matawi yangu;

20Utukufu wangu utakuwa mpya kwangu,[#Mwa 49:24]

Na uta wangu hurejezwa upya mkononi mwangu.

21Watu walitega masikio kunisikiliza, na kungoja,

Wakanyamaa kimya wapate sikia mashauri yangu.

22Hawakunena tena baada ya kusikia maneno yangu;

Matamko yangu yakadondoka juu yao.

23Walikuwa wakiningojea kama kungojea mvua;

Wakafunua vinywa vyao sana kama mvua ya masika.

24Walipokata tamaa nikacheka nao;

Na mwanga wa uso wangu hawakuuangusha.

25Niliwachagulia njia, nikakaa kama mkuu wao.

Nikakaa kama mfalme katika jeshi la askari,

Mfano wa awafarijiye hao waombolezao.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania