Ayu 33

Ayu 33

Elihu Amkemea Ayubu

1Walakini, Ayubu, nakuomba usikilize matamko yangu,[#Ayu 13:6]

Ukayasikilize maneno yangu yote.

2Tazama basi, nimefunua kinywa changu,

Ulimi wangu umenena kinywani mwangu.

3Maneno yangu yatatamka uelekevu wa moyo wangu;[#1 The 1:3]

Na hayo niyajuayo midomo yangu itayanena kwa unyofu.

4Roho ya Mungu imeniumba,[#Mwa 2:7]

Na pumzi za Mwenyezi hunipa uhai.

5Kwamba waweza, nijibu;

Yapange maneno yako sawasawa mbele yangu, usimame.

6Tazama, mimi ni mbele ya Mungu kama ulivyo wewe;[#Ayu 9:32]

Mimi nami nilifinyangwa katika udongo.

7Tazama, utisho wangu hautakutia hofu wewe,[#Ayu 13:21]

Wala sitakulemea kwa uzito.

8Hakika umenena masikioni mwangu,

Nami nimesikia sauti ya maneno yako, ukisema,

9Mimi ni safi, sina makosa;[#Ayu 10:7]

Sina hatia, wala hapana uovu ndani yangu;

10Tazama, yuaona sababu za kufarakana nami,[#Ayu 13:24]

Hunihesabu kuwa ni adui yake;

11Hunitia miguu yangu katika mkatale,[#Ayu 13:27]

Na mapito yangu yote huyapeleleza.

12Tazama, nitakujibu, katika neno hili huna haki;[#Mhu 7:20]

Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.

13Nawe kwani kumnung’unikia,[#Isa 45:9]

Kwa vile asivyotoa hesabu ya mambo yake yote?

14Kwa kuwa Mungu hunena mara moja,

Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.

15Katika ndoto, katika maono ya usiku,[#Ayu 4:13]

Usingizi mzito uwajiliapo watu,

Katika usingizi kitandani;

16Ndipo huyafunua masikio ya watu,

Na kuyatia muhuri mafundisho yao,

17Ili amwondoe mtu katika makusudio yake,

Na kumfichia mtu kiburi;

18Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni,

Na uhai wake usiangamie kwa upanga.

19Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake,[#Kum 8:5; Zab 94:12,13]

Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake;

20Hata roho yake huchukia chakula,

Na nafsi yake huchukia nyama nzuri.

21Nyama ya mwili wake huliwa, isionekane;[#Zab 102:5]

Na mifupa yake isiyoonekana yatokea nje.

22Naam, nafsi yake inakaribia shimoni,

Na uhai wake unakaribia waangamizi.

23Kwamba akiwapo malaika pamoja naye,[#2 Nya 36:15,16; Mal 2:7]

Mkalimani, mmoja katika elfu,

Ili kumwonyesha binadamu hayo yampasayo;

24Ndipo amwoneapo rehema, na kusema,[#Rum 3:24]

Mwokoe asishuke shimoni;

Mimi nimeuona ukombozi.

25Nyama ya mwili wake itakuwa laini kuliko ya mtoto;

Huzirudia siku za ujana wake;

26Yeye humwomba Mungu, naye akamtakabalia;[#2 Fal 20:2-5; Zab 6:1-9]

Hata auone uso wake kwa furaha;

Naye humrejezea mtu haki yake.

27Yeye huimba mbele ya watu, na kusema,

Mimi nimefanya dhambi, na kuyapotosha hayo yaliyoelekea,

Wala sikulipizwa jambo hilo;

28Yeye ameikomboa nafsi yangu isiende shimoni,

Na uhai wangu utautazama mwanga.

29Tazama, hayo yote ni Mungu anayeyafanya,

Mara mbili, naam, hata mara tatu, kwa mtu,

30Ili kurudisha roho yake itoke shimoni,[#Zab 40:2; Zek 9:11]

Ili atiwe mwanga kwa mwanga wa walio hai.

31Angalia sana, Ee Ayubu, unisikilize;

Nyamaza, mimi nitasema.

32Kama una neno la kusema, nijibu;[#2 Kor 1:24]

Nena, kwani nataka kukuhesabia kuwa na haki.

33Kama sivyo, unisikilize mimi;[#Zab 34:11]

Nyamaza, nami nitakufunza hekima.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania