Ayu 35

Ayu 35

Elihu Alaani Haki ya Kibinafsi

1Tena Elihu akajibu na kusema,

2Je! Wewe wadhani kwamba haya ni haki yako,

Au je! Wasema, Haki yangu ni zaidi kuliko ya Mungu,

3Maana wasema, Kutakuwa na faida gani kwako wewe?

Tena, Nitapata faida gani, kuliko nikifanya dhambi?

4Mimi nitakujibu,

Na hawa wenzio pamoja nawe.

5Ziangalie mbingu ukaone;

Na mawingu yaangalie, yaliyo juu kuliko wewe.

6Ikiwa umefanya dhambi, umefanya nini juu yake?[#Ayu 22:2-3]

Yakiwa makosa yako yameongezeka, wamfanyia nini yeye?

7Ikiwa u mwenye haki, wampa kitu gani?[#Mit 9:12; Rum 11:35]

Au yeye hupokea nini mkononi mwako?

8Uovu wako waweza kumwumiza mtu kama wewe;

Na haki yako yaweza kumfaa mwanadamu.

9Kwa sababu ya wingi wa jeuri wao hulia;[#Kut 2:23; Neh 5:5; Ayu 24:12; Zab 12:5; Lk 18:3-7]

Walilia msaada kwa sababu ya mkono wa wakuu.

10Wala hapana asemaye, Yuko wapi Mungu Muumba wangu,[#Mhu 12:1; Isa 51:13; 1 Pet 4:19; Zab 42:8; Mdo 16:25]

Awapaye nyimbo wakati wa usiku;

11Atufundishaye zaidi ya hayawani wa nchi,[#Ayu 32:8; Zab 8:6; 1 Yoh 5:20]

Na kutufanya wenye hekima kuliko ndege za angani?

12Hulia huko, lakini hapana ajibuye,[#Mit 1:28]

Kwa sababu ya kiburi cha watu waovu.

13Hakika Mungu hatasikia ubatili,

Wala Mwenyezi hatauangalia.

14Sembuse usemapo wewe ya kuwa humwangalii,

Hiyo daawa i mbele yake, nawe wamngojea!

15Lakini sasa, kwa sababu yeye hakukujilia katika hasira zake,

Wala hauangalii sana unyeti;

16Ndiposa Ayubu hufunua kinywa chake kwa ubatili;[#Ayu 34:35,37]

Huongeza maneno pasipo maarifa.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania