Ayu 39

Ayu 39

1Je! Wajua majira ya kuzaa kwao mbuzi-mwitu walio majabalini?

Au waweza kusema majira ya kuzaa kulungu?

2Je! Waweza kuhesabu miezi yao watakayoitimiza?

Au je! Wajua majira ya kuzaa kwao?

3Wao hujiinamisha, kuzaa watoto wao,

Watupa taabu zao.

4Watoto wao wa katika hali nzuri, hukua katika bara wazi;

Huenda zao, wala hawarudi tena.

5Ni nani aliyempeleka punda-milia aende huru?

Au je! Ni nani aliyemfungulia vifungo punda-mwitu?

6Ambaye nimeifanya nyika kuwa nyumba yake,[#Ayu 24:5; Yer 2:24; Hos 8:9]

Na nchi ya chumvi kuwa makao yake.

7Yeye hudharau mshindo wa mji,

Wala hasikii kelele zake msimamizi.

8Upana wa milima ni malisho yake,

Hutafuta-tafuta kila kitu kilicho kibichi.

9Je! Nyati atakubali kukutumikia?

Au atakaa katika zizi lako?

10Je! Waweza kumfunga nyati kwa kamba matutani?

Au, yeye atayalima mabonde nyuma yako?

11Je! Utamtumaini kwa sababu ana nguvu nyingi?

Au, utamwachia yeye kazi yako?

12Je! Utamtumaini kwamba ataileta mbegu yako nyumbani.

Na kukusanya nafaka ya kiwanja chako cha kupuria?

13Bawa la mbuni hufurahi;

Lakini mabawa yake na manyoya yake, je! Yana huruma?

14Kwani yeye huyaacha mayai yake juu ya nchi,

Na kuyatia moto mchangani,

15Na kusahau kwamba yumkini mguu kuyavunja,

Au mnyama wa mwitu kuyakanyaga.

16yeye huyafanyia ukali makinda yake, kana kwamba si yake;[#Law 26:29; Isa 49:15; Yer 19:9; Omb 2:20; Eze 5:10]

Ijapokuwa taabu yake ni ya bure, hana hofu;

17Kwa sababu Mungu amemnyima akili,[#Ayu 35:11]

Wala hakumpa fahamu.

18Wakati anapojiinua juu aende,

Humdharau farasi na mwenye kumpanda.

19Je! Wewe ulimpa farasi uwezo wake?

Au, ni wewe uliyemvika shingo yake manyoya yatetemayo?

20Ndiwe uliyemfanya aruke kama nzige?

Fahari ya mlio wake hutisha.

21Hupara-para bondeni, na kuzifurahia nguvu zake;[#Yer 8:6]

Hutoka kwenda kukutana na wenye silaha.

22Yeye hufanyia kicho dhihaka, wala hashangai;

Wala hageuki kurudi nyuma mbele ya upanga.

23Podo humpigia makelele,

Mkuki ung’aao na fumo.

24Huimeza nchi kwa ukali wake na ghadhabu;

Wala hasimami kwa sauti ya baragumu.

25Kila ipigwapo baragumu yeye husema, Aha!

Naye husikia harufu ya vita toka mbali,

Mshindo wa maakida, na makelele.

26Je! Mwewe huruka juu kwa akili zako,

Na kuyanyosha mabawa yake kwenda kusini?

27Je! Tai hupaa juu kwa amri yako,[#Yer 49:16]

Na kufanya kioto chake mahali pa juu?

28Hukaa jabalini, ndiko kwenye malazi yake,

Juu ya genge la jabali, na ngomeni.

29Toka huko yeye huchungulia mawindo;

Macho yake huyaangalia toka mbali.

30Makinda yake nayo hufyonza damu;[#Mt 24:28; Lk 17:37]

Na kwenye maiti ndiko aliko.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania