The chat will start when you send the first message.
1Ndipo Ayubu akamjibu BWANA, na kusema.
2Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote,[#Yer 32:17; Mt 3:9; Mk 14:36; Lk 1:37; Efe 3:20]
Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.
3Ni nani huyu afichaye mashauri bila maarifa?[#Ayu 38:2; 1 Tim 1:7; Zab 40:5]
Kwa maana, nimesema maneno nisiyoyafahamu,
Mambo ya ajabu ya kunishinda mimi, nisiyoyajua.
4Sikiliza, nakusihi, nami nitanena;[#Ayu 38:3]
Nitakuuliza neno, nawe niambie.
5Nilikuwa nimesikia habari zako, kwa kusikia kwa masikio;[#Rum 10:17; Hes 12:8,9; Isa 6:1]
Bali sasa jicho langu linakuona.
6Kwa sababu hiyo najichukia nafsi yangu, na kutubu
Katika mavumbi na majivu.
7Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.
8Basi sasa, jitwalieni ng’ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu.[#Hes 23:1; Ebr 10:4; Mt 5:24; Mwa 20:17; Ebr 7:25; Yak 5:16]
9Basi Elifazi, Mtemani, na Bildadi, Mshuhi, na Sofari, Mnaamathi, wakaenda, wakafanya kama vile BWANA alivyowaamuru; naye BWANA akamridhia Ayubu.
10Kisha BWANA akaugeuza uteka wa Ayubu, hapo alipowaombea rafiki zake; BWANA naye akampa Ayubu mara mbili kuliko hayo aliyokuwa nayo kwanza.[#Ayu 1:1-3; Isa 40:2]
11Ndipo wakamwendea nduguze wote, waume kwa wake, nao wote waliojuana naye hapo zamani, wakala chakula pamoja naye katika nyumba yake; nao wakamlilia na kumtuza moyo katika habari za huo uovu wote BWANA aliouleta juu yake; kila mtu akampa kipande cha fedha, na pete ya dhahabu kila mmoja.[#Ayu 19:13]
12Basi hivyo BWANA akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng’ombe elfu, na punda wake elfu.[#Ayu 8:7; 1:3]
13Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu.
14Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu.
15Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume.
16Kisha baada ya mambo hayo Ayubu akaishi miaka mia na arobaini, naye akawaona wanawe, na wana wa wanawe, hata vizazi vinne.[#Ayu 5:26]
17Basi Ayubu akafa, mzee sana mwenye kujawa na siku.[#Mwa 25:8]