Yos 9

Yos 9

Wagibeoni Wajiokoa kwa Hila

1Kisha ikawa hapo wafalme wote waliokaa ng’ambo ya pili ya Yordani, hapo penye nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika upande wa pwani yote ya bahari kubwa kuikabili Lebanoni, yaani, huyo Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, waliposikia habari ya mambo hayo;[#Hes 34:6; Mwa 15:18,21; Kut 3:17; 23:23; Kum 7:1]

2ndipo walipojikutanisha pamoja wenyewe kwa wenyewe, ili kupigana na Yoshua, na hao Israeli, kwa nia moja.[#1 Nya 20:1; Zab 2:1,2; 83:3,5; Mit 11:21; Isa 8:9-12; Yoe 3:9-12; Mdo 4:26-28]

3Lakini wenyeji wa Gibeoni waliposikia habari ya hayo yote Yoshua aliyokuwa amewatenda watu wa Yeriko, na wa Ai,[#Yos 10:2; 2 Sam 21:1,2; Yos 6:27]

4wao wakatenda kwa hila, nao wakaenda na kujifanya kama ndio wajumbe, wakaenda na magunia makuukuu juu ya punda zao, na viriba vya mvinyo vilivyokuwa vikuukuu vilivyoraruka-raruka, na kutiwa viraka;[#Ayu 32:19; Mt 9:17; Lk 5:37,38]

5na viatu vilivyotoboka na kushonwa-shonwa katika miguu yao, na mavao makuukuu waliyokuwa wanavaa; tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka na kuingia koga.

6Nao wakamwendea Yoshua hata maragoni huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi.[#Yos 5:10]

7Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, Labda mwakaa kati yetu; nasi tutawezaje kufanya agano nanyi?[#Kut 23:32; 34:12; Kum 7:2; Yos 11:19; Amu 2:2]

8Nao wakamwambia Yoshua, Sisi tu watumishi wako. Yoshua akawauliza, Ninyi ni nani? Nanyi mwatoka wapi?[#Kum 20:11; 2 Fal 10:5]

9Nao wakamwambia, Sisi watumishi wako twatoka nchi iliyo mbali sana, kwa sababu ya jina la BWANA, Mungu wako; kwa kuwa sisi tumesikia sifa zake, na habari ya hayo yote aliyofanya huko Misri,[#Kum 20:15; Kut 15:14; Yos 2:10]

10na habari ya hayo yote aliyowatenda wale wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa huko ng’ambo ya pili ya Yordani, maana huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, aliyekuwa huko Ashtarothi.[#Hes 21:21-35]

11Kisha wazee wetu, na wenyeji wote wa nchi yetu, walinena nasi na kutuambia, Chukueni vyakula mkononi mwenu kwa ajili ya safari, mwende mkawalaki watu hao, na kuwaambia, Sisi tu watumishi wenu; basi sasa fanyeni agano nasi.

12Huu mkate wetu tuliutwaa ukali moto katika nyumba zetu, siku hiyo tuliyotoka kuja kwenu, uwe chakula chetu; lakini sasa, tazama, umekauka, na kuingia koga;

13na viriba vyetu hivi, tulivyovitia divai, vilikuwa ni vipya; sasa, tazama, vimeraruka-raruka; na haya mavazi yetu na viatu vyetu vimekuwa vikuukuu kwa vile tulivyokuja safari ya mbali sana.

14Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa BWANA.[#Hes 27:21; Amu 1:1; 1 Sam 22:10; 23:10,11; 30:8; 2 Sam 2:1; 5:19; Isa 30:1,2]

15Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia.[#2 Sam 21:2]

16Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao.

17Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikilia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu.[#Yos 18:25; Ezr 2:25]

18Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung’unikia hao wakuu.[#Zab 15:4]

19Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa BWANA, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa.

20Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia.[#2 Sam 21:1; Eze 17:13-18; Zek 5:3,4; Mal 3:5]

21Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia.[#Kum 29:11]

22Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mwakaa kati yetu?

23Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.[#Mwa 9:25]

24Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo BWANA, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili.[#Kut 23:32; Hes 33:51-56; Kum 7:1,2; 20:15-17; Kut 15:14]

25Basi sasa, tazama, sisi tu mkononi mwako; basi kama uonavyo kuwa ni vyema na haki kwako wewe kututenda, tutende vivyo.[#Mwa 16:6]

26Naye akawafanyia hivyo, na kuwaokoa na mkono wa wana wa Israeli, ili wasiwaue.

27Siku iyo hiyo Yoshua akawafanya kuwa ni wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano, na kwa ajili ya madhabahu ya BWANA, hata siku hii ya leo, katika mahali hapo atakapopachagua.[#Kum 12:5; 1 Fal 8:29; 9:7; 2 Nya 7:12,20; Zab 78:68]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania