Yud 1

Yud 1

Salamu

1Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo, ndugu yake Yakobo, kwa hao walioitwa, waliopendwa katika Mungu Baba, na kuhifadhiwa kwa ajili ya Yesu Kristo.[#Mt 13:55; Mk 6:3]

2Mwongezewe rehema na amani na upendano.[#2 Pet 1:2]

3Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.[#1 Tim 1:18; 2 Pet 1:5; 2:21]

4Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.[#Gal 2:4; 2 Pet 2:1]

Hukumu kwa Waalimu Waongo

5Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kujua haya yote, ya kwamba Bwana, akiisha kuwaokoa watu katika nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasioamini.[#Kut 12:51; Hes 14:29-30,35; 1 Kor 10:5; 2 Pet 1:12]

6Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.[#Mwa 6:1; Yn 8:44; 2 Pet 2:4,9]

7Kama vile Sodoma na Gomora na miji iliyokuwa kando-kando, waliofuata uasherati kwa jinsi moja na hawa, wakaenda kufuata mambo ya mwili yasiyo ya asili, imewekwa kuwa dalili, wakiadhibiwa katika moto wa milele.[#Mwa 19:1-24; 2 Pet 2:6,19]

8Kadhalika na hawa, katika kuota kwao, huutia mwili uchafu, hukataa kutawaliwa, na kuyatukana matukufu.[#2 Pet 2:10]

9Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee.[#Kum 34:6; Dan 10:13,21; 12:1; Zek 3:2; Ufu 21:7; 2 Pet 2:11]

10Lakini watu hawa huyatukana mambo wasiyoyajua, na mambo wayatambuayo kwa asili wajiharibu kwayo kama wanyama wasio na akili.[#2 Pet 2:12]

11Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora.[#Mwa 4:3-8; Hes 22:1-35; 16:1-35; 31:16; 2 Pet 2:15]

12Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung’olewa kabisa;[#Eze 34:8; 2 Pet 2:13]

13ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.[#Isa 57:20; 2 Pet 2:17]

14Na Henoko, mtu wa saba baada ya Adamu, alitoa maneno ya unabii juu ya hao, akisema, Angalia, Bwana alikuja na watakatifu wake, maelfu maelfu,[#Mwa 5:18,21-24; Kum 33:2; Zek 14:5]

15ili afanye hukumu juu ya watu wote, na kuwaadhibisha wote wasiomcha Mungu, kwa ajili ya kazi zao zote za upotevu walizozitenda bila kumcha Mungu, na kwa ajili ya maneno magumu yote ambayo hao wenye dhambi wasiomcha Mungu wameyanena juu yake.[#Mt 25:31]

16Watu hawa ni wenye kunung’unika, wenye kulalamika, waendao kwa tamaa zao, na vinywa vyao vyanena maneno makuu mno ya kiburi, wakipendelea watu wenye cheo kwa ajili ya faida.[#2 Pet 2:10,18]

Maonyo na Himizo

17Bali ninyi, wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo,[#2 Pet 3:2]

18ya kwamba waliwaambia ya kuwa, Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa zao wenyewe za upotevu.[#2 Pet 3:3,5; 1 Tim 4:1]

19Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na Roho.[#1 Kor 2:14]

20Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu,[#Kol 2:7; 1 The 5:11]

21jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele.

22Wahurumieni wengine walio na shaka,

23na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili.[#Amo 4:11; Zek 3:2; Yak 5:19; Ufu 3:4]

Baraka

24Yeye awezaye kuwalinda ninyi msijikwae, na kuwasimamisha mbele ya utukufu wake bila mawaa katika furaha kuu;[#1 The 5:23; Flp 1:10; 2 Pet 3:14]

25Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina.[#Rum 16:27; 1 Tim 1:17; 2 Pet 3:18]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania