The chat will start when you send the first message.
1Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni[#Mt 11:23; 2 Sam 1:19; 1 Nya 28:2]
Kwa wingu katika hasira yake!
Ameutupa toka mbinguni hata nchi
Huo uzuri wa Israeli;
Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake
Katika siku ya hasira yake.
2Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo,[#Zab 89:39]
Wala hakuona huruma;
Ameziangusha ngome za binti Yuda
Katika ghadhabu yake;
Amezibomoa hata nchi
Ameunajisi ufalme na wakuu wake.
3Ameikata pembe yote ya Israeli[#Ayu 16:15; Zab 74:11]
Katika hasira yake kali;
Ameurudisha nyuma mkono wake wa kuume
Mbele ya hao adui,
Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao,
Ulao pande zote.
4Ameupinda upinde wake kama adui,[#Isa 63:10]
Amesimama na mkono wake wa kuume kama mtesi;
Naye amewaua hao wote
Waliopendeza macho;
Katika hema ya binti Sayuni
Amemimina kani yake kama moto.
5Bwana amekuwa mfano wa adui,[#Yer 52:13]
Amemmeza Israeli;
Ameyameza majumba yake yote,
Ameziharibu ngome zake;
Tena amemzidishia binti Yuda
Matanga na maombolezo.
6Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu,[#Zab 80:12; Sef 3:18; Isa 5:5; 1:8]
Kana kwamba ni ya bustani tu;
Ameziharibu sikukuu zake;
BWANA amezisahauzisha katika Sayuni
Sikukuu za makini na sabato;
Naye amewadharau mfalme na kuhani
Katika uchungu wa hasira yake.
7Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake,[#Zab 78:59-61; Eze 7:20; Isa 64:10,11; Mik 3:12; Yer 7:12-14; Mt 24:2; Zab 74:4]
Amepachukia patakatifu pake;
Amezitia katika mikono ya hao adui
Kuta za majumba yake;
Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya BWANA
Kama katika siku ya kusanyiko la makini.
8BWANA amekusudia kuuharibu[#Isa 34:11; Amo 7:7]
Ukuta wa binti Sayuni;
Ameinyosha hiyo kamba,
Hakuuzuia mkono wake usiangamize;
Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza;
Zote pamoja hudhoofika.
9Malango yake yamezama katika nchi;[#Kum 28:36; 2 Fal 25:7; 2 Nya 15:3; Zab 74:9; Amo 8:11,12; Mik 3:6,7]
Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja;
Mfalme wake na wakuu wake wanakaa
Kati ya mataifa wasio na sheria;
Naam, manabii wake hawapati maono
Yatokayo kwa BWANA.
10Wazee wa binti Sayuni huketi chini,[#Ayu 2:13; Omb 4:5; Isa 47:1-5]
Hunyamaza kimya;
Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao,
Wamejivika viunoni nguo za magunia;
Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao
Kuielekea nchi.
11Macho yangu yamechoka kwa machozi,[#Zab 6:7; Ayu 16:13]
Mtima wangu umetaabika;
Ini langu linamiminwa juu ya nchi
Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu;
Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao,
Huzimia katika mitaa ya mji.
12Wao huwauliza mama zao,
Zi wapi nafaka na divai?
Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa
Katika mitaa ya mji,
Hapo walipomiminika nafsi zao
Vifuani mwa mama zao.
13Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini,[#Ayu 5:1; Dan 9:12]
Ee Binti Yerusalemu?
Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji,
Ee bikira binti Sayuni?
Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari,
Ni nani awezaye kukuponya?
14Manabii wako wameona maono kwa ajili yako[#Isa 58:1]
Ya ubatili na upumbavu
Wala hawakufunua uovu wako,
Wapate kurudisha kufungwa kwako;
Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako
Na sababu za kuhamishwa.
15Hao watu wote wapitao[#1 Fal 9:8; Zab 48:2]
Hukupigia makofi;
Humzomea binti Yerusalemu,
Na kutikisa vichwa vyao;
Je! Mji huu ndio ulioitwa, Ukamilifu wa uzuri,
Furaha ya dunia yote?
16Juu yako adui zako wote[#Zab 56:2; 35:21]
Wamepanua vinywa vyao;
Huzomea, husaga meno yao,
Husema, Tumemmeza;
Hakika siku hii ndiyo tuliyoitazamia;
Tumeipata, tumeiona.
17BWANA ameyatenda aliyoyakusudia; amelitimiza neno lake,[#Law 26:16; Zab 38:16; Kum 28:15,43,44; Omb 1:5]
Aliloliamuru siku za kale;
Ameangusha hata chini,
Wala hakuona huruma;
Naye amemfurahisha adui juu yako,
Ameitukuza pembe ya watesi wako.
18Mioyo yao ilimlilia Bwana;[#Yer 14:17; Omb 1:16]
Ee ukuta wa binti Sayuni!
Machozi na yachuruzike kama mto
Mchana na usiku;
Usijipatie kupumzika;
Mboni ya jicho lako isikome.
19Inuka, ulalamike usiku,[#Mk 13:35; Zab 62:8; Isa 51:20; Omb 4:1; Nah 3:10]
Mwanzo wa makesha yake;
Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana;
Umwinulie mikono yako;
Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa,
Mwanzo wa kila njia kuu.
20Tazama, BWANA, uangalie,[#Kut 32:11; Law 26:29; Kum 28:53; Yer 19:9; Omb 4:10,13]
Ni nani uliyemtenda hayo!
Je! Wanawake wale mazao yao,
Watoto waliowabeba?
Je! Kuhani na nabii wauawe
Katika patakatifu pa Bwana?
21Kijana na mzee hulala chini[#2 Nya 36:17]
Katika njia kuu;
Wasichana wangu na wavulana wangu
Wameanguka kwa upanga;
Umewaua katika siku ya hasira yako;
Umeua, wala hukuona huruma.
22Umeziita kama katika siku ya mkutano wa makini;[#Zab 31:13; Yer 46:5; Hos 9:12]
Hofu zangu zije pande zote;
Wala hapana hata mmoja aliyepona wala kusalia
Katika siku ya hasira ya BWANA;
Hao niliowabeba na kuwalea
Huyo adui yangu amewakomesha.