Omb 5

Omb 5

Ombi la Kuhurumiwa

1Ee BWANA, kumbuka yaliyotupata;

Utazame na kuiona aibu yetu.

2Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni;

Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri.

3Tumekuwa yatima waliofiwa na baba;

Mama zetu wamekuwa kama wajane.

4Tumekunywa maji yetu kwa fedha;

Kuni zetu twauziwa.

5Watufuatiao wa juu ya shingo zetu;

Tumechoka tusipate raha yo yote.

6Tumewapa hao Wamisri mkono;[#Mwa 24:2; Yer 50:15; Hos 12:1]

Na Waashuri nao, ili tushibe chakula.

7Baba zetu walitenda dhambi hata hawako;[#Yer 16:12; Eze 18:2; Mt 23:32]

Na sisi tumeyachukua maovu yao.

8Watumwa wanatutawala;

Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.

9Twapata chakula kwa kujihatarisha nafsi zetu;

Kwa sababu ya upanga wa nyikani.

10Ngozi yetu ni nyeusi kama tanuu;

Kwa sababu ya hari ya njaa ituteketezayo.

11Huwatia jeuri wanawake katika Sayuni;[#Isa 13:16]

Na mabikira katika miji ya Yuda.

12Wakuu hutungikwa kwa mikono yao;

Nyuso za wazee hazipewi heshima.

13Vijana huyachukua mawe ya kusagia;[#Amu 16:21]

Na watoto hujikwaa chini ya kuni.

14Wazee wameacha kwenda langoni;[#2 Fal 25:18]

Na vijana kwenda ngomani.

15Furaha ya mioyo yetu imekoma;

Machezo yetu yamegeuka maombolezo.

16Taji ya kichwa chetu imeanguka;

Ole wetu! Kwa kuwa tumetenda dhambi.

17Kwa sababu hiyo mioyo yetu imezimia;[#Ayu 17:7; Zab 6:7]

Kwa ajili ya hayo macho yetu hayaoni vema.

18Kwa ajili ya mlima Sayuni ulio ukiwa,

Mbweha hutembea juu yake.

19Wewe, BWANA, unadumu milele;

Kiti chako cha enzi ni tangu kizazi hata kizazi.

20Mbona watusahau sikuzote;

Na kutuacha muda huu mwingi?

21Ee BWANA, utugeuze kwako, nasi tutageuka; Zifanye mpya siku zetu kama siku za kale.

22Isipokuwa wewe umetukataa kabisa;

Nawe una hasira nyingi sana juu yetu.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania