The chat will start when you send the first message.
1BWANA akamwambia Musa, akisema,
2Sema na Haruni, na wanawe, na wana wote wa Israeli, ukawaambie; Neno hili ndilo aliloliamuru BWANA, akisema,
3Mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli atakayechinja ng’ombe, au mwana-kondoo, au mbuzi, ndani ya marago, au atakayemchinja nje ya marago,
4wala hamleti mlangoni pa hema ya kukutania, ili amtoe kuwa matoleo kwa BWANA mbele ya hema ya BWANA; mtu huyo atahesabiwa kuwa ana hatia ya damu; amemwaga damu; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake;[#Kum 12:5; Zab 32:2; Rum 4:6; 5:13; Mwa 17:14]
5ili kusudi wana wa Israeli walete sadaka zao, wazichinjazo mashambani, naam, wazilete kwa BWANA, mpaka mlango wa hema ya kukutania, kwa huyo kuhani, ili wazichinje ziwe sadaka za amani kwa BWANA.[#Mwa 21:33; 22:2; Kum 12:2; 1 Fal 14:22,23; 2 Fal 17:10; Eze 20:28; 22:9]
6Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya BWANA, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za BWANA.[#Kut 29:18; Law 4:31; Hes 18:17]
7Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi.[#Kum 32:17; 2 Nya 11:15; Zab 106:37; Mdo 7:42,43; 1 Kor 10:20; Kut 34:15; Kum 31:16]
8Nawe utawaambia, Mtu awaye yote katika nyumba ya Israeli, au miongoni mwa wageni, wanaokaa nao, atoaye sadaka ya kuteketezwa au dhabihu,
9wala haileti mlangoni pa hema ya kukutania, ili aisongeze kwa BWANA basi mtu huyo atatengwa na watu wake.
10Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake.[#Mwa 9:4; Law 7:26-27; 19:26; Kum 12:16,23; 15:23; 1 Sam 14:33; Law 26:17; Yer 44:11; Eze 15:7]
11Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.[#Ebr 9:22; Mk 14:24; Rum 5:9; Efe 1:7; Kol 1:14; 1 Pet 1:2; 1 Yoh 1:7]
12Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu.
13Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga.[#Kum 12:16; 15:23; 1 Sam 14:32-34; Eze 24:7]
14Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.[#Mwa 9:4]
15Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni; ndipo atakapokuwa safi.[#Kut 22:31; Kum 14:21; Eze 4:14]
16Lakini kwamba hazifui, wala haogi mwili, ndipo atakapochukua uovu wake.[#Hes 19:20; Ebr 9:28]