The chat will start when you send the first message.
1Kisha BWANA akanena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia,[#Kut 23:10-11]
2Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika Sabato kwa ajili ya BWANA.[#Kut 23:10; Law 26:34,35; 2 Nya 36:21]
3Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipelee shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake;
4lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ni Sabato kwa BWANA; usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako la mizabibu.
5Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde; utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi.[#2 Fal 19:29; Isa 37:30]
6Na hiyo Sabato ya nchi itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa mgeni wako akaaye pamoja nawe;
7na kwa hayawani wako, na kwa wanyama walio katika nchi yako; maongeo yote yatakuwa ni chakula chao.
8Nawe utajihesabia Sabato saba za miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za Sabato saba za miaka kwenu, maana miaka arobaini na kenda.
9Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo baragumu yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote.[#Law 23:24; 16:20,30]
10Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile kwenu; nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake.[#Kut 20:2; Ezr 6:3; Isa 49:24,25; Yer 34:8,15,17; Lk 4:19; Gal 5:1; Hes 36:4; #25:10 Neno hili Yubile, kwa asili, maana yake ni Baragumu iliyopigwa kila mwaka wa hamsini.]
11Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabibu za mizabibu isiyopelewa.
12Kwa kuwa ni yubile; utakuwa mwaka mtakatifu kwenu; mtakula maongeo yake yatokayo shambani.
13Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake.[#Law 27:24; Hes 36:4]
14Tena kama ukimwuzia jirani yako cho chote, au kununua cho chote mkononi mwa jirani yako, msidanganyane wenyewe kwa wenyewe;[#Law 19:13; 1 Sam 12:3; Zab 10:18; Mik 2:2; 1 Kor 6:8]
15kwa hesabu ya miaka iliyo baada ya yubile, ndivyo utakavyonunua kwa jirani yako, na kama hesabu ya miaka ya mavuno ndivyo atakavyokuuzia wewe.
16Kama hesabu ya miaka ilivyo ni nyingi ndivyo utakavyoongeza bei yake, na kama hesabu ya miaka ilivyo ni chache ndivyo utakavyopunguza bei yake; kwani yeye akuuzia mavuno kama hesabu yake ilivyo.
17Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Mit 14:31; 22:22; Yer 7:6; Eze 22:29; 1 The 4:6]
18Kwa sababu hii zitendeni amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzifanya; nanyi mtakaa katika hiyo nchi salama.[#Law 26:5; Kum 12:10; Zab 4:8; Mit 1:33; Yer 23:6]
19Nayo nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba, na kuketi humo salama.
20Na kama mkisema, Je! Mwaka wa saba tutakula nini? Angalieni hatutapanda mbegu, wala kukusanya maongeo yetu;[#Mt 6:25; Hes 11:4-13; 2 Fal 6:15]
21ndipo nitawaamria baraka yangu iwe juu yenu mwaka wa sita, nayo utazaa matunda hesabu ya miaka mitatu.[#Kut 16:29; Kum 28:8; Zab 33:12; 119:2; Mit 3:33; 8:32; 1 Tim 4:8]
22Na mwaka wa nane mtapanda mbegu, na kuyala yale matunda, akiba hiyo ya zamani, hata mwaka wa kenda, hata matunda yake yatakapoletwa ndani, mtakula hiyo akiba ya zamani.[#2 Fal 19:29; Yos 5:11]
23Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu.[#Kum 32:43; 2 Nya 7:20; Zab 24:1; 85:1; Isa 8:8; Hos 9:3; Yoe 2:18; Zab 119:19; 1 Pet 2:11]
24Nanyi mtatoa ukombozi kwa ajili ya nchi, katika nchi yote ya milki yenu.
25Kwamba nduguyo amekuwa maskini, na kuuza sehemu ya milki yake, ndipo jamaa yake aliye karibu naye atakuja, naye ataikomboa ile aliyoiuza nduguye.[#Rut 2:20; 3:2]
26Na kama mtu hana atakayeikomboa, naye mwenyewe amepata mali na kujiona kuwa anayo ya kutosha kuikomboa;
27ndipo na aihesabu hiyo miaka ya kuuzwa kwake, na kilichozidi kumrudishia huyo mtu aliyeinunua; naye atairejea milki yake.
28Lakini asipoweza kujipatia mwenyewe, ndipo hiyo iliyouzwa itakaa mkononi mwake huyo aliyeinunua, hata mwaka wa yubile; na katika yubile itatoka, naye atairejea milki yake.
29Tena kwamba mtu anauza nyumba ya kukaa, iliyo ndani ya mji wenye kuta, ndipo ana ruhusa kuikomboa katika mwaka mmoja mzima baada ya kuiuza; atakuwa na amri ya kuikomboa muda wa mwaka mzima.
30Na kama haikukombolewa katika muda wa mwaka mzima, ndipo hiyo nyumba iliyo ndani ya mji wenye kuta itathibitishwa milele kuwa ya huyo aliyeinunua, katika vizazi vyake; nayo haitatoka katika yubile.
31Lakini nyumba za vijiji, ambavyo havikuzingirwa na kuta, zitahesabiwa pamoja na mashamba ya nchi; nazo zina ruhusa ya kukombolewa, nazo zitatoka katika yubile.
32Pamoja na hayo, miji ya Walawi, nyumba za miji ya milki yao, Walawi wana ruhusa ya kuzikomboa majira yo yote.[#Yos 21:2]
33Tena kama mtu mmoja wa hao Walawi akikomboa, ndipo nyumba iliyouzwa, na mji wa milki yake, itatoka katika yubile; maana, hizo nyumba za miji ya Walawi ni milki yao kati ya wana wa Israeli.
34Lakini konde la malisho ya miji yao lisiuzwe kwa kuwa ni milki yao ya daima.[#Mdo 4:36]
35Na ikiwa ndugu yako amekuwa maskini, na mkono wake umelegea kwako, ndipo utamsaidia, atakaa nawe kama mgeni, na msafiri.[#Kum 15:7-8; Zab 37:26; Mit 14:31; Lk 6:35; Mdo 11:29; Rum 12:18; 1 Yoh 3:17]
36Usitake riba kwake wala faida, bali mche Mungu wako, ili ndugu yako akae nawe.[#Kut 22:25; Kum 23:19; Neh 5:7; Zab 15:5; Mit 28:8; Eze 18:8,13,17]
37Usimpe fedha yako upate riba, wala usimpe vyakula vyako kwa kujitakia faida.[#Kut 22:25; Kum 23:19-20]
38Mimi ndimi BWANA, Mungu wako, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili niwape nchi ya Kanaani, nipate kuwa Mungu wenu.
39Tena kwamba nduguyo amekuwa maskini pamoja nawe, akajiuza kwako; usimtumikishe mfano wa mtumwa;[#Kut 21:2-6; 22:3; Kum 15:12-18; 1 Fal 9:22; 2 Fal 4:1; Yer 34:14]
40kwako wewe atakuwa mfano wa mtumishi aliyeajiriwa, au mfano wa msafiri; naye atatumika kwako hata mwaka wa yubile;
41ndipo atakapotoka kwako aende zake, yeye na wanawe pamoja naye, naye atairejea jamaa yake mwenyewe, tena atairejea milki ya baba zake.
42Kwa kuwa hao ni watumishi wangu, niliowaleta watoke nchi ya Misri; wasiuzwe mfano wa watumwa.[#Rum 6:22; 1 Kor 7:23]
43Usitawale juu yake kwa nguvu; ila umche Mungu wako.[#Kut 1:13,14; 2:23; 3:7,9; 5:14; Isa 47:6; Efe 6:9; Kol 4:1; Kut 1:17,21; Kum 25:18; Mal 3:5]
44Tena katika habari za watumwa wako na wajakazi wako, utakaokuwa nao; mataifa walio kando-kando yenu, katika hao mtanunua watumwa na wajakazi.
45Tena katika wana wa wageni wakaao kati yenu mtajinunulia, na katika jamaa zao walio pamoja nanyi, waliowazaa katika nchi yenu; wao watakuwa milki yenu.
46Nanyi mtawafanya kuwa urithi kwa watoto wenu baada yenu, wawe milki yao; siku zote mtatwaa watumwa wenu katika hao; lakini msitawale kwa nguvu juu ya ndugu zenu, hao wana wa Israeli, wenyewe kwa wenyewe.
47Tena kama mgeni au mtu akaaye nawe akitajirika, na nduguyo amekuwa maskini karibu naye, akajiuza kwa huyo mgeni, au kwa huyo akaaye kwako, au kwa ukoo wa jamaa ya huyo mgeni;
48baada ya kuuzwa aweza kukombolewa; mtu mmoja miongoni mwa ndugu zake ana ruhusa kumkomboa;
49au mjomba wake, au mwana wa mjomba wake, ana ruhusa ya kumkomboa, au mtu awaye yote aliye karibu naye wa jamaa yake, ana ruhusa ya kumkomboa; au kwamba yeye mwenyewe amepata mali, ana ruhusa ya kujikomboa mwenyewe.
50Naye atafanya hesabu na huyo aliyemnunua, tangu mwaka huo aliojiuza hata mwaka wa yubile; na ile bei ya kuuzwa kwake itakuwa kama hesabu ya hiyo miaka ilivyo; atakuwa pamoja naye kama majira ya mtumishi aliyeajiriwa yalivyo.
51Kwamba ikali imesalia miaka mingi, kama hesabu yake ilivyo ndivyo atakavyolipa bei ya ukombozi wake, katika hiyo fedha ambayo alinunuliwa kwayo.
52Tena kwamba imesalia miaka michache tu hata mwaka wa yubile, ndipo atafanya hesabu naye, kama hesabu ya miaka yake ilivyo, ndivyo atakavyolipa tena bei ya ukombozi wake.
53Kama mtumishi aliyeajiriwa mwaka hata mwaka, ndivyo atakavyokuwa pamoja naye; asitawale juu yake kwa nguvu mbele ya macho yako.
54Tena kwamba hakukombolewa kwa njia hizi mojawapo, ndipo atatoka katika mwaka wa yubile, yeye, na watoto wake pamoja naye.
55Kwa kuwa wana wa Israeli ni watumishi; ni watumishi wangu niliowaleta watoke katika nchi ya Misri; mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.