The chat will start when you send the first message.
1Msifanye sanamu yo yote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lo lote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.[#Kut 20:4,5; Law 19:4; Kum 4:16-19; 5:8; 16:21-22; 27:1; Isa 44:9-20; Zab 97:7]
2Zishikeni Sabato zangu, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi BWANA.
3Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya;[#Kum 11:13-15; 28:1-14]
4ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.[#Kum 28:12; Isa 30:23]
5Tena kupura nafaka kwenu kutaendelea hata wakati wa kuvuna zabibu, na kuvuna zabibu kutaendelea hata wakati wa kupanda mbegu; nanyi mtakula chakula chenu na kushiba, na kuketi katika nchi yenu salama.[#Kum 11:15; Yoe 2:19,26; Ayu 11:18; Eze 34:25]
6Nami nitawapa amani katika nchi, tena mtalala wala hapana atakayewatia hofu; nami nitawakomesha wanyama wabaya katika nchi yenu, wala hautapita upanga katika nchi yenu.[#1 Nya 22:9; Isa 45:7; Zab 3:5; Yer 30:10; Yn 14:27; Rum 5:1; 2 Fal 17:25; Eze 5:17; 14:15,17; Yos 23:10]
7Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga.
8Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga.
9Nami nitawaelekezea uso wangu, na kuwapa uzazi mwingi, na kuwaongeza; nami nitalithibitisha agano langu pamoja nanyi.[#Kut 2:25; 2 Fal 13:23; Mwa 17:6,7]
10Nanyi mtakula akiba ya zamani mliyoiweka siku nyingi, tena hayo ya zamani mtayatoa, ili myaweke yaliyo mapya.
11Nami nitaiweka maskani yangu kati yenu; wala roho yangu haitawachukia.[#Eze 37:26; Kum 32:19]
12Nami nitakwenda kati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu.[#2 Kor 6:16; Efe 2:21; Ebr 3:6; Eze 11:20]
13Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu, niliyewaleta mtoke katika nchi ya Misri, ili msiwe watumwa wao; nami nimeivunja miti ya kongwa lenu, nikawaendesha mwende sawasawa.[#Eze 34:27]
14Lakini msiponisikiza, wala hamtaki kuyafanya maagizo hayo yote;[#Kum 28:15]
15nanyi mkizikataa amri zangu, na roho yenu ikichukia hukumu zangu, hata ikawa hamtaki kuyafanya maagizo yangu yote, bali mwalivunja agano langu;[#2 Fal 17:15]
16mimi nami nitawatenda jambo hili; nitaamrisha uje juu yenu utisho, hata kifua kikuu na homa, zitakazoharibu macho yenu, na kuidhoofisha roho; nanyi mtapanda mbegu yenu bure, kwa kuwa adui zenu wataila.[#Kum 28:22; 1 Sam 2:33; Ayu 31:8]
17Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye.[#Amu 2:14; Zab 106:41; 53:5]
18Tena ikiwa baada ya hayo hamtaki kunisikiza, ndipo nitawaadhibu zaidi mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.[#1 Sam 2:5]
19Nami nitakivunja kiburi cha uwezo wenu; nami nitazifanya mbingu zenu kuwa kama chuma, na nchi yenu kuwa kama shaba;[#1 Sam 4:10; Isa 25:11]
20na nguvu zenu mtazitumia bure; kwa kuwa nchi yenu haitazaa mazao yake, wala miti ya nchi haitazaa matunda yake.[#Zab 127:1; Isa 49:4; Kum 28:18; Hag 1:10]
21Nanyi ikiwa mwaenenda kinyume changu, wala hamtaki kunisikiza; nitaleta mapigo mara saba zaidi juu yenu, kama dhambi zenu zilivyo.
22Nami nitaleta wanyama wakali kati yenu, ambao watawanyang’anya watoto wenu, na kuwaharibu wanyama wenu wa kufugwa, na kuwapunguza muwe wachache hesabu yenu; na njia zenu zitakuwa ni ukiwa.[#Kum 32:24; 2 Fal 17:25; Yer 15:3; Amu 5:6; 2 Nya 15:5; Zek 7:14]
23Tena kama hamtaki kurejezwa upya kwangu mimi kwa mambo haya, bali mwaendelea kunishikia kinyume; ndipo mimi nami nitaendelea kuwashikia ninyi kinyume;[#Yer 5:3]
24nami nitawapiga, naam mimi, mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.[#2 Sam 22:27]
25Nami nitaleta upanga juu yenu, utakaopatiliza kisasi cha hilo agano; nanyi mtakutanishwa ndani ya miji yenu; nami nitaleta tauni kati yenu; nanyi mtatiwa mkononi mwa adui.[#Eze 6:3; Kum 28:22; Hes 14:12; 16:49; Amo 4:10]
26Hapo nitakapovunja tegemeo lenu la mkate, wanawake kumi wataoka mikate yenu katika tanuu moja, nao watawapa mikate yenu tena kwa kupima kwa mizani; nanyi mtakula, lakini hamtashiba.[#Isa 3:1; Mik 6:14]
27Tena ikiwa baada ya hayo yote hamtaki kunisikiza, bali mwaenenda kwa kunishikia kinyume;
28ndipo nami nitakwenda kwa kuwashikia ninyi kinyume katika ghadhabu yangu; nami nitawaadhibu mara saba kwa dhambi zenu.[#Isa 59:18]
29Nanyi mtakula nyama ya miili ya wana wenu, na nyama ya miili ya binti zenu mtaila.[#2 Fal 6:29]
30Nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka, na kuziangusha sanamu zenu za jua, nami nitaitupa mizoga yenu juu ya mizoga ya sanamu zenu; na roho yangu itawachukia.[#2 Nya 34:3; 2 Fal 23:20; Zab 78:59]
31Nami nitaifanya miji yenu iwe maganjo, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitasikia harufu ya manukato yenu yapendezayo.[#Neh 2:3; Yer 5:10; 22:5; Zab 74:1-8; Yer 26:6,9; Omb 1:10; Eze 9:6]
32Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia.[#Yer 9:11; 25:11]
33Nanyi nitawatapanya-tapanya katika mataifa, nami nitaufuta upanga nyuma yenu; na nchi yenu itakuwa ni ukiwa, na miji yenu maganjo.[#Kum 4:27; 28:64; Zab 44:11; Eze 12:15; 20:23; Zek 7:14]
34Hapo ndipo nchi itakapozifurahia Sabato zake, wakati itakapokuwa hali ya ukiwa, nanyi mtakapokuwa katika nchi ya adui zenu; ndipo nchi itakapopumzika, na kuzifurahia Sabato zake.[#Law 25:2-4; 2 Nya 36:21]
35Wakati wote itakapokuwa na ukiwa, itapumzika; ni hayo mapumziko ambayo haikuwa nayo katika Sabato zenu, hapo mlipokaa katika nchi hiyo.
36Tena hao wa kwenu watakaobaki, nitawatilia woga mioyoni mwao, katika hizo nchi za adui zao; na sauti ya jani lililopeperushwa itawakimbiza; nao watakimbia, kama mtu akimbiavyo upanga; nao wataanguka hapo ambapo hapana afukuzaye.[#Mwa 35:5; Yos 2:9-11; Eze 21:7; Mit 28:1]
37Nao wataangukiana wenyewe kwa wenyewe, kama mbele ya upanga, hapo ambapo hapana afukuzaye; wala hamtakuwa na nguvu za kusimama mbele ya adui zenu.[#Amu 7:22; Isa 10:4; Amu 2:14]
38Nanyi mtaangamia kati ya mataifa, na nchi ya adui zenu itawameza.
39Na watu wa kwenu watakaobaki watafifia kwa ajili ya uovu wao, katika hizo nchi za adui zenu; tena watafifia kwa ajili ya uovu wa baba zao, pamoja nao.[#Neh 1:9; Yer 3:25; 20:12]
40Nao wataukiri uovu wao, na uovu wa baba zao, katika maasi yao waliyoasi juu yangu, tena ya kuwa kwa sababu wameendelea kunishikia kinyume,[#Hes 5:7; 1 Fal 8:33; Ayu 34:31; Mit 28:13; Yer 3:12; Lk 15:18; 1 Yoh 1:9]
41mimi nami nimeendelea kuwashikia kinyume wao, na kuwatia katika nchi ya adui zao; lakini hapo, kama mioyo yao isiyokuwa tohara ikinyenyekea, nao wakubali adhabu ya uovu wao;[#Yer 9:25; Eze 44:7; Mdo 7:51; Rum 2:29; Kol 2:11; 1 Fal 21:29; 2 Nya 12:6]
42ndipo nitakapokumbuka agano langu pamoja na Yakobo, tena agano langu na Isaka, tena agano langu na Ibrahimu nitalikumbuka; nami nitaikumbuka nchi hiyo.[#Mwa 17:7-8; 26:3-4; 28:13-14; Kut 2:24; 6:5; Zab 106:5; Eze 16:60; Zab 136:23]
43Nchi nayo itaachwa na wao, nayo itazifurahia Sabato zake, itakapokuwa ukiwa pasipokuwa na wao; nao wataikubali adhabu ya uovu wao; kwa sababu, naam, ni kwa sababu wamezikataa hukumu zangu, na roho zao zimezichukia amri zangu.
44Lakini pamoja na hayo yote, watakapokuwa katika nchi ya adui zao, mimi, sitawatupa, wala sitawachukia, niwaangamize kabisa, na kulivunja agano langu pamoja nao; kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wao;[#Kum 4:31]
45lakini kwa ajili yao nitalikumbuka agano la baba zao, niliowaleta watoke katika nchi ya Misri mbele ya macho ya mataifa, ili kwamba niwe Mungu wao; mimi ndimi BWANA.[#Rum 11:28; Eze 20:9]
46Hizi ni amri na hukumu na sheria, BWANA alizozifanya kati ya yeye na hao wana wa Israeli katika huo mlima wa Sinai kwa mkono wa Musa.[#Kum 33:4; Yn 1:17]