Mt 20

Mt 20

Wafanya kazi katika Shamba la Mizabibu

1Kwa maana ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu.[#Mt 21:33]

2Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu.

3Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi;

4na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda.

5Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile.

6Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?

7Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.

8Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza.[#Law 19:13; Kum 24:15]

9Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari.

10Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari.

11Basi wakiisha kuipokea, wakamnung’unikia mwenye nyumba,

12wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.

13Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?

14Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.

15Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema?[#Rum 9:16,21; Mt 6:23]

16Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.[#Mt 19:30; Mk 10:31; Lk 13:30]

Yesu asema juu ya Kifo chake na Kufufuka kwake

17Hata Yesu alipokuwa akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia,[#Mk 10:32-34; Lk 18:31-33]

18Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe;[#Mt 16:21; 17:22,23]

19kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeledi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka.

Ombi la Mama wa Yakobo na Yohana

20Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno.[#Mk 10:35-45; #Mt 10:2]

21Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako.[#Mt 19:28]

22Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza.[#Mt 26:39; Yn 18:11; Lk 12:50]

23Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu.

24Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili.[#Lk 22:24-26]

25Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha.[#Lk 22:25-26]

26Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;[#Mt 23:11; Mk 9:35; Lk 22:26]

27na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu;

28kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.[#Lk 22:27; Flp 2:7; 1 Tim 2:6]

Yesu Aponya Vipofu Wawili

29Hata walipokuwa wakitoka Yeriko mkutano mkubwa wakamfuata.[#Mk 10:46-52; Lk 18:35-43]

30Na tazama, vipofu wawili wameketi kando ya njia, nao waliposikia ya kwamba Yesu anapita, walipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi![#Mt 15:22]

31Mkutano wakawakaripia, wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti, wakisema, Uturehemu, Bwana, mwana wa Daudi!

32Yesu akasimama, akawaita, akasema, Mnataka niwafanyie nini?

33Wakamwambia, Bwana, twataka macho yetu yafumbuliwe.

34Yesu akawahurumia, akawagusa macho yao; mara wakapata kuona, wakamfuata.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania