The chat will start when you send the first message.
1Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake,[#Mt 7:28; 11:1; 13:53; 19:1]
2Mnajua ya kuwa baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, na Mwana wa Adamu atasalitiwa asulibiwe.[#Mk 14:1,2; Lk 22:1,2; #Kut 12:1-27; Mt 20:18]
3Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa;
4wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.
5Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.
6Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma,[#Mk 14:3-9; Lk 7:36-50; Yn 12:1-8]
7mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani.[#Lk 7:37-38]
8Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu?
9Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini.
10Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi.[#Lk 11:7]
11Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote.[#Kum 15:11]
12Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu.
13Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake.
14Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani,[#Mk 14:10,11; Lk 22:3-6]
15akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha.[#Zek 11:12; Yn 11:57; #26:15 Yapata kama shilingi 90.]
16Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.[#1 Tim 6:9,10]
17Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?[#Mk 14:12-16; Lk 22:7-13; #Kut 12:18-20]
18Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.[#Mt 21:3]
19Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka.
20Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara.[#Mk 14:17-26; Lk 22:14-23; Yn 13:21-26]
21Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti.
22Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana?
23Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti.[#Zab 41:10]
24Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.
25Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.
26Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu[#Mt 14:19; 1 Kor 11:23-25]
27Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;
28kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.[#Kut 24:8; Yer 31:31-34; Zek 9:11]
29Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.
30Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.[#Zab 113—118; Lk 22:39; Yn 18:1]
31Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.[#Mk 14:27-31; Lk 22:31-34; #Zek 13:7; Yn 16:32]
32Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.[#Mt 28:7,16]
33Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.
34Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu.[#Yn 13:38]
35Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.[#Mt 26:56]
36Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.[#Mk 14:32-42; Lk 22:40-46]
37Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.[#Ebr 5:7]
38Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.[#Zab 43:5; Yn 12:27]
39Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.[#Yn 18:11; Ebr 5:8]
40Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?
41Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.[#Ebr 2:14; 4:15]
42Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe.
43Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito.
44Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.[#2 Kor 12:8]
45Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi.
46Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia.[#Yn 14:31]
47Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu.[#Mk 14:43-50; Lk 22:47-53; Yn 18:3-12]
48Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni.
49Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu.
50Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu.
51Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.
52Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.[#Mwa 9:6; Ufu 13:10]
53Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?[#Yoe 3:11]
54Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?
55Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang’anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate.[#Lk 19:47; 21:37]
56Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.[#Mt 26:31]
57Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee.[#Mk 14:53-72; Lk 22:54-71; Yn 18:12-27]
58Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho.
59Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua;
60wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi.
61Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu.[#Yn 2:19-21]
62Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?
63Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.[#Mt 27:12]
64Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.[#Dan 7:13; Zab 110:1; Mt 16:27; 24:30]
65Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake;[#Law 24:16; Mt 9:3; Yn 10:33]
66mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa.[#Yn 19:7]
67Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi,[#Isa 50:6]
68wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga?
69Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya.
70Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo.
71Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti.
72Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu.
73Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha.
74Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo.
75Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.[#Mt 26:34]