The chat will start when you send the first message.
1Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua;[#Mk 15:1; Lk 22:66; Yn 18:28]
2wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali.[#Lk 23:1; Yn 18:31,32]
3Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.[#Mdo 1:18-19; Mt 26:15]
4Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.
5Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.[#Mdo 1:18; 2 Sam 17:23]
6Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu.[#Mk 12:41]
7Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.
8Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo.[#Mdo 1:19]
9Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima;[#Zek 11:12-13; Yer 32:6-9]
10wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.
11Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema.[#Mk 15:2-5; Lk 23:2,3; Yn 18:29-38]
12Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno.[#Mt 26:63; Isa 53:7]
13Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?
14Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana.[#Yn 19:9]
15Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka.[#Mk 15:6-15; Lk 23:13-25; Yn 18:39—19:1]
16Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba.
17Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo?
18Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.[#Yn 11:47,48; 12:19]
19Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake.
20Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu.
21Basi liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema, Baraba.
22Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe.
23Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe.
24Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.[#Kum 21:6-9]
25Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.[#Mdo 5:28]
26Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.
27Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima.[#Mk 15:16-19; Yn 19:2,3; #Praitorio maana yake ni Nyumba ya Uliwali.]
28Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu.
29Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!
30Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani.[#Isa 50:6]
31Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.[#Mk 15:20-41; Lk 23:26,33-49; Yn 19:16-30]
32Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake.
33Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa,
34wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa.[#Zab 69:22]
35Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.][#Zab 22:19]
36Wakaketi, wakamlinda huko.
37Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI.
38Wakati uo huo wanyang’anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto.[#Isa 53:12]
39Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema,[#Zab 22:8; 109:25]
40Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani.[#Mt 26:61; Yn 2:19]
41Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.
42Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini.
43Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.[#Zab 22:9]
44Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.
45Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa.
46Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?[#Zab 22:2]
47Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya.
48Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha.[#Zab 69:22]
49Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.
50Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.
51Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;[#Kut 26:31-33; Ebr 10:19,20]
52makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;
53nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.[#Mdo 26:23; Dan 12:2]
54Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.
55Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia.[#Lk 8:2-3]
56Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.[#Mt 20:20]
57Hata ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu;[#Mk 15:42-47; Lk 23:50-55; Yn 19:38-42; #Kut 34:25]
58mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe.
59Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya kitani safi,
60akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.[#Isa 53:9]
61Na pale walikuwapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi.
62Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato,
63wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka.[#Mt 16:21; 27:40; 12:40; 17:23; 20:19; Mk 8:31; 9:31; 10:33-34; Lk 9:22; 18:31-33]
64Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.
65Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo.
66Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.[#Dan 6:17]