The chat will start when you send the first message.
1Mwanzo wa Injili ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.
2Kama ilivyoandikwa katika nabii Isaya,[#Mal 3:1; Mt 11:10; Yn 3:28; #Mt 3:1-12; Lk 3:1-18; Yn 1:19-30]
Tazama, namtuma mjumbe wangu
Mbele ya uso wako,
Atakayeitengeneza njia yako.
3Sauti ya mtu aliaye nyikani,[#Isa 40:3]
Itengenezeni njia ya Bwana,
Yanyosheni mapito yake.
4Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi.
5Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao.
6Na Yohana alikuwa amevaa singa za ngamia na mshipi wa ngozi kiunoni mwake, akala nzige na asali ya mwitu.[#2 Fal 1:8; Zek 13:4]
7Akahubiri akisema, Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya viatu vyake.[#Mdo 13:25]
8Mimi niliwabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu.
9Ikawa siku zile, Yesu alikuja kutoka Nazareti ya Galilaya, akabatizwa na Yohana katika Yordani.[#Lk 2:51; #Mt 3:13-17; Lk 3:21-22; Yn 1:31-34]
10Mara alipopanda kutoka majini, akaona mbingu zinapasuka, na Roho, kama hua, akishuka juu yake;
11na sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.[#Mwa 22:2; Zab 2:7; Isa 42:1; Mt 3:17; 12:18; Mk 9:7; Lk 3:22]
12Mara Roho akamtoa aende nyikani.[#Mt 4:1-11; Lk 4:1-13]
13Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia.[#Zab 91:13; Yn 1:51]
14Hata baada ya Yohana kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu,[#Mt 4:12-17; Lk 4:14,15]
15akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.[#Mt 3:2; Gal 4:4]
16Naye alipokuwa akipita kando ya bahari ya Galilaya, akamwona Simoni na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.[#Mt 4:18-22; Lk 5:1-11]
17Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.[#Mt 13:47]
18Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.
19Akaendelea mbele kidogo, akamwona Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, nao pia walikuwa chomboni, wakizitengeneza nyavu zao.
20Mara akawaita, wakamwacha baba yao Zebedayo ndani ya chombo pamoja na watu wa mshahara, wakaenda, wakamfuata.
21Wakashika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha.[#Lk 4:31-37; #Mt 4:13]
22Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi.[#Mt 7:28,29]
23Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti,
24akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza?[#Mk 5:7; Zab 16:10]
25Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke.
26Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka.[#Mk 9:26]
27Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii!
28Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.
29Na mara walipotoka katika sinagogi, walifika nyumbani kwa Simoni na Andrea, pamoja na Yakobo na Yohana.[#Mt 8:14-16; Lk 4:38-41]
30Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake.
31Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.
32Hata kulipokuwa jioni, na jua limekwisha kuchwa, walikuwa wakimletea wote waliokuwa hawawezi, na wenye pepo.
33Na mji wote ulikuwa umekusanyika mlangoni.
34Akaponya wengi waliokuwa na maradhi mbalimbali, akatoa pepo wengi, wala hakuwaacha pepo kunena, kwa sababu walimjua.[#Lk 4:41; Mdo 16:17,18]
35Hata alfajiri na mapema sana akaondoka, akatoka akaenda zake mahali pasipokuwa na watu, akaomba huko.[#Lk 4:42-44]
36Simoni na wenziwe wakamfuata;
37nao walipomwona wakamwambia, Watu wote wanakutafuta.
38Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea.
39Akaenda akihubiri katika masinagogi yao, katika nchi yote ya Galilaya, na kutoa pepo.[#Mt 4:23; 9:35]
40Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.[#Mt 8:2-4; Lk 5:12-16]
41Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka, takasika.
42Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika.
43Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara,[#Mk 3:12; 7:36]
44akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao.[#Law 14:1-32; Law 13:49]
45Lakini akatoka, akaanza kuhubiri maneno mengi, na kulitangaza lile neno, hata Yesu asiweze tena kuingia mjini kwa wazi; bali alikuwako nje mahali pasipokuwa na watu, wakamwendea kutoka kila mahali.