The chat will start when you send the first message.
1Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi.[#Ezr 4:1-5; Neh 2:10; Zab 2:1-4; Mdo 5:17]
2Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto?
3Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.[#Neh 2:10,19]
4Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho;[#Zab 123:3,4; Isa 53:3; Lk 16:14; 1 Sam 17:26; Zab 79:12; Mit 3:34; Hos 12:14]
5wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga.[#Zab 59:5-13; 69:27; Yer 18:23; 2 Tim 4:14]
6Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi.
7Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno;
8wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.[#Zab 2:1-3; Isa 8:9,10; Mdo 23:12,13]
9Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu, tena tukaweka walinzi, mchana na usiku, kwa sababu yao, ili kuwapinga.[#Ayu 22:27; Zab 50:15; Mt 26:41]
10Wakasema Yuda, Nguvu zao wachukuao mizigo zimedhoofika, na kifusi tele zipo; tusiweze kuujenga ukuta.
11Nao adui zetu wakasema, Hawatajua wala kuona, hata tutakapokuja kati yao, na kuwaua, na kuikomesha kazi hiyo.
12Kisha ikawa, Wayahudi walipokuja, wale waliokaa karibu nao, wakatuambia mara kumi, Kutoka kila mahali mtakaporejea watatushambulia.
13Basi, nikaweka watu, mahali pa chini pa nafasi iliyokuwa nyuma ya ukuta, mahali palipokuwa wazi, kwa kadiri ya jamaa zao, nikawaweka wenye panga zao, na mikuki yao, na pinde zao.
14Nikatazama, nikaondoka, nikawaambia wakuu, na mashehe, na watu wengine waliobaki, Msiwaogope; mkumbukeni Bwana, aliye mkuu mwenye kuogofya, mkawapiganie ndugu zenu, na wana wenu, na binti zenu, na wake zenu, na nyumba zenu.[#Hes 14:9; Kum 1:29; 10:17; Ayu 37:22; Ebr 12:20,21,28,29; 2 Sam 10:12]
15Kisha ikawa, adui zetu waliposikia ya kuwa tumekwisha kupata habari, na ya kuwa Mungu amelibatilisha shauri lao, ndipo sisi sote tukarudi ukutani, kila mtu kwa kazi yake.[#Ayu 5:12; Zab 33:10]
16Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda.
17Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono wake wa pili alishika silaha yake;[#1 Kor 16:13; Efe 6:10]
18nao wajenzi, kila mtu alikuwa na upanga wake, umefungwa ubavuni mwake, ndivyo alivyojenga. Na yeye aliyepiga baragumu alikuwa karibu na mimi.
19Nikawaambia wakuu, na mashehe na watu wengine; Kazi hii ni nyingi, tena kubwa, nasi tumetawanyika juu ya ukuta, kila mtu mbali na mwenzake;
20basi mahali po pote mtakaposikia sauti ya baragumu, enendeni huko, mkatujie; Mungu wetu atatupigania.[#Kut 14:14; Yos 23:10; Kum 1:30; 3:22]
21Hivyo tukajitia katika kazi hiyo; na nusu yao waliishika mikuki, tangu alfajiri hata nyota zikatokea.
22Kadhalika, wakati ule ule, nikawaambia watu, Kila mtu na akae ndani ya Yerusalemu pamoja na mtumishi wake, wapate kuwa walinzi wetu wakati wa usiku, na kufanya kazi wakati wa mchana.
23Basi mimi, na ndugu zangu, na watumishi wangu, na watu wa ulinzi walionifuata, hatukuvua nguo zetu hata mmoja; kila mtu alikwenda kuteka maji akichukua silaha yake.