The chat will start when you send the first message.
1Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa BWANA; BWANA aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa BWANA ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago.[#Kut 15:23,24; 16:2,3,7,9; Kum 9:22; Omb 3:39; Law 10:2; 2 Fal 1:12]
2Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba BWANA, na ule moto ukakoma.[#Yak 5:16]
3Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa BWANA ukawaka kati yao.
4Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?[#Kut 12:38; 1 Kor 10:6]
5Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;[#Kut 16:3; Flp 3:19; Mt 6:24-34; Rum 8:7]
6lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu.
7Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola.[#Kut 16:31; Mwa 2:12]
8Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya.
9Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.[#Kut 16:13-15]
10Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za BWANA zikawaka sana; Musa naye akakasirika.
11Musa akamwambia BWANA, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu?[#Kut 17:4; Kum 1:12; Yer 15:10,18; Yer 20:7-18; Mal 3:14; 2 Kor 11:28]
12Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao?[#Isa 40:11; Eze 34:23; Yn 10:11; Isa 49:23; 1 The 2:7; Mwa 22:16; 26:3; Kut 13:5]
13Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula.[#2 Fal 4:43; Mt 15:33; Mk 8:4]
14Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda.[#Kut 18:18]
15Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.[#1 Fal 19:4; Ayu 6:8-10; Yon 4:3; Sef 3:15]
16Kisha BWANA akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe.[#Kut 24:1,9]
17Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako.[#Mwa 11:5; Kut 19:20; 1 Sam 10:6; 2 Fal 2:5; Ayu 32:8; 38:36; Yoe 2:28]
18Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa BWANA, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo BWANA atawapa nyama, nanyi mtakula.[#Kut 19:10; 16:7; Mdo 7:39]
19Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini;
20lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa BWANA aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani?
21Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima.
22Je! Makundi ya kondoo na ng’ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha?[#2 Fal 7:2; Mt 15:33; Mk 6:37]
23BWANA akamwambia Musa, Je! Mkono wa BWANA umepungua urefu wake? Sasa utaona kwamba neno langu litatimizwa kwako, au sivyo.[#Isa 50:2; Eze 12:25; 24:14]
24Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya BWANA; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema.
25Ndipo BWANA akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena.[#Kut 34:5; 40:38; Hes 12:5; 2 Fal 2:15; 1 Sam 10:5,6; Yoe 2:29; Mdo 2:17,18; 1 Kor 14:1]
26Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini.[#1 Sam 20:26; Yer 36:5]
27Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.
28Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze.[#Mk 9:38; Yn 3:26]
29Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa BWANA wangekuwa manabii na kama BWANA angewatia roho yake.[#Mdo 26:29; 1 Kor 14:5]
30Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli.
31Kisha upepo ukavuma kutoka kwa BWANA, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi.[#Zab 78:26]
32Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote.[#Kut 16:36; Eze 45:11]
33Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za BWANA ziliwaka juu ya watu, BWANA akawapiga watu kwa pigo kuu mno.[#Zab 78:30; 106:14]
34Jina la mahali pale likaitwa Kibroth-hataava; maana, ni hapo walipowazika hao watu waliotamani.[#Kum 9:22]
35Kutoka hapo Kibroth-hataava watu wakasafiri kwenda Haserothi; wakakaa huko Haserothi.[#Hes 33:17; Kum 1:1]