The chat will start when you send the first message.
1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu wakati wake upasao.[#Law 3:11; 21:6,8; Mal 1:7,12]
3Nawe utawaambia, Hii ndiyo sadaka isongezwayo kwa moto mtakayomsongezea BWANA; wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu, wawili kila siku, wawe sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.[#Kut 29:38]
4Mwana-kondoo mmoja utamsongeza asubuhi, na mwana-kondoo wa pili utamsongeza jioni;[#Kut 12:6]
5pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta ya kupondwa.[#Kut 16:36; 29:38-42; Law 2:1; Hes 15:4]
6Ni sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, iliyoamriwa huko katika mlima wa Sinai iwe harufu ya kupendeza, sadaka ya kusongezwa kwa BWANA kwa moto.
7Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwana-kondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia BWANA katika mahali hapo patakatifu.[#Kut 29:42; 30:9; Law 23:13; Hes 15:5-10; Isa 57:1]
8Na mwana-kondoo wa pili utamsongeza wakati wa jioni; kama ile sadaka ya unga iliyosongezwa asubuhi, na kama sadaka yake ya kinywaji, ndivyo utakavyoisongeza, ni sadaka ya kusongezwa kwa moto, ni harufu ya kupendeza kwa BWANA.
9Tena katika siku ya Sabato watasongezwa wana-kondoo wawili, waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, pamoja na sehemu ya kumi mbili za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, pamoja na sadaka yake ya kinywaji;
10hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila Sabato, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.[#Eze 46:4]
11Tena katika mianzo ya miezi yenu mtamsongezea BWANA sadaka ya kuteketezwa; nayo ni ng’ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, saba;[#Hes 10:10; 1 Sam 20:5; 1 Nya 23:31; 2 Nya 2:4; Ezr 3:5; Neh 10:33; Isa 1:13,14; Eze 45:17; Hos 2:11; Kol 2:16]
12pamoja na sehemu ya kumi tatu za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa kila ng’ombe; na sehemu ya kumi mbili za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa huyo kondoo mume mmoja;[#Hes 15:4; 29:10; Eze 46:5,7]
13na sehemu ya kumi moja ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga kwa kila mwana-kondoo; kuwa sadaka ya kuteketezwa ya harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa njia ya moto.
14Tena sadaka zake za vinywaji zitakuwa nusu ya hini ya divai kwa ng’ombe, na sehemu ya tatu ya hini kwa kondoo mume, na robo ya hini kwa mwana-kondoo; hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi katika miezi yote ya mwaka.
15Tena mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa BWANA itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
16Tena, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, ni pasaka ya BWANA.[#Kut 12:1-13; Kum 16:1-2; Law 23:5; Eze 45:21; Mt 26:2,17; Lk 22:7]
17Siku ya kumi na tano ya mwezi huo patakuwa na sikukuu; mkate usiotiwa chachu utaliwa muda wa siku saba.[#Kut 12:14-20; 23:15; 34:18; Kum 16:3-8; Law 23:6]
18Siku ya kwanza patakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi;[#Law 23:7]
19lakini mtaisongeza sadaka kwa njia ya moto, sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA; ng’ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; watakuwa wakamilifu kwenu;[#Law 22:20; Hes 29:8; Kum 15:21]
20pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta; mtasongeza sehemu ya kumi tatu kwa ng’ombe mmoja, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume;
21na sehemu ya kumi moja utasongeza kwa kila mwana-kondoo, wale wana-kondoo saba;
22tena mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.[#Law 16:18; Rum 8:3; Gal 4:4; Ebr 9:12; 10:1]
23Mtasongeza wanyama hao zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, iliyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.
24Mtasongeza sadaka kwa mfano huu kila siku muda wa siku saba, chakula cha sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa BWANA; itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.[#2 Kor 2:15; Efe 5:2]
25Na siku ya saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi.[#Kut 12:16; 13:6; Law 23:8]
26Tena katika siku ya malimbuko, hapo mtakapomsongezea BWANA sadaka ya unga mpya katika sikukuu yenu ya majuma mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi;[#Kut 23:16; 34:22; Kum 16:9-12; Law 23:10,15; Mit 3:9; Mdo 2:1]
27lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa BWANA; ng’ombe waume wadogo wawili, kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba;[#Law 23:18,19]
28pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa kila ng’ombe, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume,
29na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo, wa wale wana-kondoo saba;
30na mbuzi mume mmoja, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
31Zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, mtasongeza wanyama hao (watakuwa wakamilifu kwenu), pamoja na sadaka zake za vinywaji.