Hes 34

Hes 34

Mipaka ya Nchi

1Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

2Waagize wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapoingia nchi ya Kanaani, (hii ndiyo nchi itakayowaangukia kuwa urithi, maana, hiyo nchi ya Kanaani kama mipaka yake ilivyo,)[#Mwa 17:8; Kum 1:7; Zab 78:55; 105:11]

3ndipo upande wenu wa kusini utakuwa tangu bara ya Sini kupita kando ya Edomu, na mpaka wenu wa kusini utakuwa tangu mwisho wa Bahari ya Chumvi kuelekea mashariki;[#Yos 15:1; Eze 47:13; Mwa 14:3; Yos 3:16]

4kisha mpaka wenu utageuka kwenda upande wa kusini wa kukwelea kwake Akrabimu, kisha kupita kwendelea Sini; na kutokea kwake kutakuwa kuelekea upande wa kusini wa Kadesh-barnea; kisha utaendelea mpaka Hasar-adari, na kufikilia Azmoni;[#Hes 32:8]

5kisha mpaka utageuka kutoka Azmoni kwendelea kijito cha Misri, na kutokea kwake kutakuwa hapo baharini.[#Mwa 15:18; 1 Fal 8:65; Isa 27:12]

6Kisha mpaka wenu wa upande wa magharibi mtakuwa na bahari kubwa na mpaka wake; hii ndiyo mpaka wenu upande wa magharibi.

7Kisha mpaka wenu wa upande wa kaskazini utakuwa ni huu; kutoka bahari kubwa mtajiandikia mlima wa Hori;

8na kutoka mlima wa Hori mtaandika mpaka kuingilia kwake Hamathi; na kutokea kwake mpaka kutakuwa hapo Sedada;[#Hes 13:21; Yos 13:5,6; 2 Sam 8:9; 2 Fal 14:25; 23:33; Isa 10:9; Yer 39:5; Eze 47:15-20]

9tena mpaka utatokea hata Zifroni, na kutokea kwake kutakuwa hapo Hasarenani; huo ndio mpaka wenu wa upande wa kaskazini.[#Eze 47:17]

10Kisha mtaandika mpaka wenu wa upande wa mashariki kutoka Hasarenani hata Shefamu;

11kisha mpaka utatelemka kutoka Shefamu mpaka Ribla, upande wa mashariki wa Aini; kisha mpaka utatelemka na kufikilia upande wa bahari ya Kinerethi upande wa mashariki;[#2 Fal 23:33; Yer 39:5; Kum 3:17; Yos 11:2; 19:35]

12kisha mpaka utatelemkia Yordani, na kutokea kwake kutakuwa hapo katika Bahari ya Chumvi; hii ndiyo nchi yenu kama mipaka yake ilivyo kuizunguka pande zote.

13Kisha Musa akawaagiza wana wa Israeli, akisema, Hii ndiyo nchi mtakayoirithi kwa kupiga kura, ambayo BWANA ameagiza wapewe watu wa zile kabila kenda, na nusu ya kabila;[#Yos 14:1-5; #Hes 26:52-56; Yos 14:1,2]

14kwa kuwa kabila ya wana wa Reubeni kwa nyumba za baba zao, na kabila ya wana wa Gadi kwa nyumba za baba zao, wamekwisha pata, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wamekwisha pata urithi wao;[#Hes 32:33; Yos 14:2,3]

15hizo kabila mbili na nusu ya kabila wamekwisha pata urithi wao huko ng’ambo ya pili ya Yordani, hapo Yeriko, upande wa mashariki, kuelekea maawio ya jua.

Viongozi wa Makabila

16Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,

17Haya ndiyo majina ya watu watakaowagawanyia nchi iwe urithi wenu; Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni.[#Kut 6:23-25]

18Kisha mtamtwaa mkuu mmoja wa kila kabila, ili waigawanye nchi iwe urithi wenu.

19Na majina ya watu hao ni haya; katika kabila ya Yuda, ni Kalebu mwana wa Yefune.[#Mwa 29:35; 49:8-10; Kum 33:7; Zab 60:7; 108:8; Hes 13:6,30; Kum 1:36]

20Na katika kabila ya wana wa Simeoni, Shemueli mwana wa Amihudi.[#Mwa 29:33; 49:5; Eze 48:24]

21Katika kabila ya Benyamini, ni Elidadi mwana wa Kisloni.[#Mwa 35:18; 49:27; Kum 33:12; Zab 68:27; 80:2]

22Na katika kabila ya wana wa Dani, mkuu, Buki mwana wa Yogli.

23Katika wana wa Yusufu; katika kabila ya wana wa Manase, mkuu, Hanieli mwana wa Efodi;[#Mwa 48:8-22; 49:22; Kum 33:13; Zab 80:1]

24na katika kabila ya wana wa Efraimu, mkuu, Kemueli mwana wa Shiftani.

25Na katika kabila ya wana wa Zabuloni, mkuu, Elisafani mwana wa Parnaki.

26Na katika kabila ya wana wa Isakari, mkuu, Paltieli mwana wa Azani.

27Na katika kabila ya wana wa Asheri, mkuu, Ahihudi mwana wa Shelomi.

28Na katika kabila ya wana wa Naftali, mkuu, Pedaheli mwana wa Amihudi.

29Hao ndio BWANA aliowaagiza wawagawanyie urithi wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani.[#Kum 32:8; Mdo 17:26]

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania