The chat will start when you send the first message.
1Mizani ya hadaa ni chukizo kwa BWANA;
Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza.
2Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu;[#Dan 4:30]
Bali hekima hukaa na wanyenyekevu.
3Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza
Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.
4Mali hazifaidii kitu siku ya ghadhabu;[#Eze 7:19; Sef 1:18; Mwa 7:1]
Bali haki huokoa na mauti.
5Haki yake mtu mkamilifu itamwongoza njia yake;
Bali mtu mwovu ataanguka kwa uovu wake.
6Haki yao wenye haki itawaokoa;[#1 Tim 4:8; Mhu 10:8]
Bali wafanyao fitina watanaswa kwa hila yao wenyewe.
7Mtu mwovu atakapokufa, taraja lake lapotea;
Na matumaini ya uovu huangamia.
8Mwenye haki huokolewa katika dhiki,
Na mtu mwovu ataiingia badala yake.
9Asiyemcha Mungu humpoteza jirani yake kwa kinywa chake;[#Ayu 8:13]
Bali wenye haki watapona kwa maarifa.
10Wenye haki wasitawipo, mji hufurahi;[#Est 8:15]
Waovu waangamiapo, watu hupiga kelele.
11Mji hutukuzwa kwa mbaraka wa mwenye haki;
Bali mji hupinduliwa kwa kinywa cha mwovu.
12Asiye na akili humdharau mwenziwe;
Bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza.
13Mwenye kitango akisingizia hufunua siri;
Bali mwenye roho ya uaminifu husitiri mambo.
14Pasipo mashauri taifa huanguka;[#1 Fal 12:1]
Bali kwa wingi wa washauri huja wokovu.
15Amdhaminiye mgeni hakosi ataumia;
Achukiaye mambo ya dhamana yu salama.
16Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima;
Na watu wakali hushika mali siku zote.
17Mwenye rehema huitendea mema nafsi yake;[#Mt 25:34]
Aliye mkali hujisumbua mwili wake.
18Mtu mwovu hupata mshahara wa udanganyifu;[#Hos 10:12; Gal 6:8,9]
Apandaye haki ana thawabu ya hakika.
19Haki huelekea uzima;
Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe.
20Wenye kuhalifu moyoni ni chukizo kwa BWANA;
Walio wakamilifu katika njia zao humpendeza.
21Hakika, mtu mwovu hatakosa adhabu;
Bali wazao wa wenye haki wataokoka.
22Kama pete ya dhahabu katika pua ya nguruwe,
Kadhalika mwanamke mzuri asiye na akili.
23Haja ya mwenye haki ni mema tu;[#Rum 2:8]
Bali kutaraji kwake mtu mwovu ni ghadhabu.
24Kuna atawanyaye, lakini huongezewa zaidi;
Kuna azuiaye isivyo haki, lakini huelekea uhitaji.
25Nafsi ya mtu mkarimu itawandishwa;[#Mt 5:7]
Anyweshaye atanyweshwa mwenyewe.
26Awanyimaye watu nafaka, watu watamlaani;[#Amo 8:5; Ayu 29:13]
Auzaye nafaka, baraka itakuwa kichwani pake.
27Atafutaye mema kwa bidii hutafuta fadhili;[#Est 7:10]
Atafutaye madhara, hayo yatamjia.
28Azitegemeaye mali zake ataanguka;[#Mk 10:24; Lk 12:21; 1 Tim 6:17; Yer 17:8]
Mwenye haki atasitawi kama jani.
29Ataabishaye nyumba yake mwenyewe ataurithi upepo;[#Mhu 5:16]
Mpumbavu atakuwa mtumwa wa mtu mwenye moyo wa akili.
30Mazao ya mwenye haki ni mti wa uzima;
Na mwenye hekima huvuta roho za watu.
31Tazama, mwenye haki atalipwa duniani;[#1 Pet 4:18; Yer 25:29]
Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi zaidi?