Mit 13

Mit 13

1Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye;[#1 Sam 2:25; Mit 9:7,8]

Bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.

2Mtu atakula mema kwa matunda ya kinywa chake;

Bali nafsi ya mtu haini itakula jeuri.

3Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake;[#Zab 39:1]

Bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu.

4Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu;

Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa.

5Mwenye haki huchukia kusema uongo;[#Kol 3:9; Rum 12:9]

Bali mtu mbaya huwa karaha, hupatwa na aibu.

6Haki humlinda yeye aliye mnyofu katika njia yake;[#Mit 11:3]

Bali ubaya humwangusha mwenye dhambi.

7Kuna mtu mwenye kujitajirisha, lakini hana kitu;

Kuna ajifanyaye kuwa maskini, lakini ana mali nyingi.

8Dia ya nafsi ya mtu ni utajiri wake;

Bali mtu maskini hasikii ogofyo lo lote.

9Nuru ya mwenye haki yang’aa sana;

Bali taa ya mtu mbaya itazimika.

10Kiburi huleta mashindano tu;

Bali hekima hukaa nao wanaoshauriana.

11Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka;[#Mit 20:21]

Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa.

12Kilichotarajiwa kikikawia kuja, moyo huugua.

Bali haja ya mtu ikipatikana, ni mti wa uzima.

13Kila alidharauye neno hujiletea uharibifu;[#2 Nya 36:16]

Bali yeye aiogopaye amri atapewa thawabu.

14Sheria ya mwenye akili ni chemchemi ya uzima,[#Mit 16:22; 15:24; 2 Sam 22:6; Zab 116:3]

Ili kuepukana na tanzi za mauti.

15Ufahamu mwema huleta upendeleo;

Bali njia ya haini huparuza.

16Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa;[#Mit 12:23]

Bali mpumbavu hueneza upumbavu.

17Mjumbe mbaya huanguka maovuni;

Bali mjumbe mwaminifu ni afya.

18Umaskini na fedheha zitampata yeye akataaye kurudiwa;[#Mit 15:5]

Bali yeye aangaliaye maonyo ataheshimiwa.

19Haja iliyopatikana ni tamu nafsini mwa mtu;

Bali kujitenga na maovu ni chukizo kwa wapumbavu.

20Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima;

Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

21Uovu huwaandamia wenye dhambi;[#Zab 32:10]

Bali mwenye haki atalipwa mema.

22Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi;[#Mhu 2:26]

Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.

23Chakula kingi chapatikana kwa ukulima wa maskini;[#Mit 12:11]

Bali viko viharibiwavyo kwa sababu ya dhuluma.

24Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanawe;[#Mit 19:18; 22:15]

Bali yeye ampendaye humrudi mapema.

25Mwenye haki hula akaishibisha nafsi yake;

Bali tumbo la mtu mbaya litaona njaa.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania