Mit 14

Mit 14

1Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake;[#Rut 4:11; Mit 24:3,4]

Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

2Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha BWANA;[#Ayu 12:4]

Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.

3Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi,[#Mit 12:6]

Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi.

4Zizi ni safi ambapo hapana ng’ombe;

Bali nguvu za ng’ombe zaleta faida nyingi.

5Shahidi mwaminifu hatasema uongo;[#Kut 20:16]

Bali shahidi wa uongo, pumzi zake ni uongo.

6Mwenye dharau hutafuta hekima, asiipate;[#Mit 17:24]

Bali maarifa huwa mepesi kwa mwenye ufahamu.

7Toka mbele ya uso wa mpumbavu,

Maana hutaona kwake midomo ya maarifa.

8Akili za mwenye busara ni kujua njia yake;[#Lk 12:20; 1 Kor 3:19]

Lakini upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.

9Wapumbavu huidharau hatia;[#Mit 1:22]

Bali upo upendeleo kwa wenye haki.

10Moyo huujua uchungu wa nafsi yake,

Wala mgeni haishiriki furaha yake.

11Nyumba ya mtu mbaya itabomolewa;[#Ayu 8:15; Mit 3:33]

Bali hema ya mwenye haki itafanikiwa.

12Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu,[#Mit 16:25; Rum 6:21]

Lakini mwisho wake ni njia za mauti.

13Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni;[#Mhu 2:2]

Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo.

14Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe;[#Mit 12:14; 2 Kor 1:12; Flp 4:7]

Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.

15Mjinga huamini kila neno;

Bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.

16Mwenye hekima huogopa, akajitenga na uovu;[#Mit 22:3]

Bali mpumbavu ana ufidhuli, na kujitumai.

17Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga;

Na mtu mwenye hila mbaya huzirwa.

18Wajinga hurithi upumbavu;

Bali wenye busara huvikwa taji ya maarifa.

19Wabaya huinama mbele ya wema,

Na wasio haki malangoni mwao wenye haki.

20Maskini huchukiwa hata na jirani yake;[#Mit 19:7]

Bali tajiri ana rafiki wengi.

21Amdharauye mwenzake afanya dhambi;[#Zab 41:1]

Bali amhurumiaye maskini ana heri.

22Je! Hawakosi wawazao mabaya?

Bali fadhili na kweli zina wao wawazao mema.

23Katika kila kazi mna faida;

Bali maneno ya midomo huleta hasara tu.

24Taji ya wenye hekima ni mali zao;

Bali upumbavu wa wajinga ni upumbavu tu.

25Shahidi wa kweli huponya nafsi za watu;

Bali atoaye uongo hudanganya.

26Kumcha BWANA ni tumaini imara;

Watoto wake watakuwa na kimbilio.

27Kumcha BWANA ni chemchemi ya uzima,[#Mit 13:14]

Ili kuepukana na tanzi za mauti.

28Utukufu wa mfalme ni wingi wa watu wake;

Bali uchache wa watu ni uharibifu wa mkuu wao.

29Asiye mwepesi wa hasira ana fahamu nyingi;[#Mit 15:18; Mt 11:29; 1 Kor 13:4,5; Yak 1:19]

Bali mwenye roho ya hamaki hutukuza upumbavu.

30Moyo ulio mzima ni uhai wa mwili;[#Ayu 5:2; Zab 112:10; Mdo 7:9; Rum 1:29; Yak 4:5]

Bali husuda ni ubovu wa mifupa.

31Amwoneaye maskini humsuta Muumba wake;[#Ayu 31:15,16; Mhu 5:8; Mit 17:5; 22:2; Mt 25:40; 1 Yoh 3:17]

Bali yeye awahurumiaye wahitaji humheshimu.

32Mtu mbaya husukumwa chini katika kutenda mabaya kwake;[#Ayu 13:15; Zab 23:4; 2 Kor 1:9; 2 Tim 4:18]

Bali mwenye haki ana matumaini katika kufa kwake.

33Hekima hukaa katika moyo wake mwenye ufahamu;

Bali yaliyo ndani ya wapumbavu hudhihirika.

34Haki huinua taifa;

Bali dhambi ni aibu ya watu wo wote.

35Upendeleo wa mfalme humwelekea mtumwa atendaye kwa busara;[#Mt 24:45-47]

Bali ghadhabu yake itakuwa juu yake aletaye aibu.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania