The chat will start when you send the first message.
1Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu,
Na kuyaweka akiba maagizo yangu;
2Hata ukatega sikio lako kusikia hekima,
Ukauelekeza moyo wako upate kufahamu;
3Naam, ukiita busara,
Na kupaza sauti yako upate ufahamu;
4Ukiutafuta kama fedha,[#Zab 19:10; Mit 3:14,15; Mt 6:19-21]
Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;
5Ndipo utakapofahamu kumcha BWANA,
Na kupata kumjua Mungu.
6Kwa kuwa BWANA huwapa watu hekima;[#Lk 21:15; Yn 6:45; Yak 1:5]
Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;
7Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili;[#Zab 84:11]
Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu;
8Apate kuyalinda mapito ya hukumu,[#1 Sam 2:9; 1 Pet 1:5; Zab 37:23,24,28,31]
Na kuhifadhi njia ya watakatifu wake.
9Ndipo utakapofahamu haki na hukumu,
Na adili, na kila njia njema.
10Maana hekima itaingia moyoni mwako,
Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;
11Busara itakulinda;[#Mit 6:22]
Ufahamu utakuhifadhi.
12Ili kukuokoa na njia ya uovu,
Na watu wanenao yaliyopotoka;
13Watu waziachao njia za unyofu,[#Yn 3:19; Efe 4:18]
Ili kuziendea njia za giza;
14Wafurahio kutenda mabaya;
Wapendezwao na upotoe wa waovu;
15Waliopotoka katika njia zao;
Walio wakaidi katika mapito yao.
16Ili kuokoka na malaya,
Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;
17Amwachaye rafiki wa ujana wake,[#Mal 2:14; Mwa 2:24]
Na kulisahau agano la Mungu wake.
18Maana nyumba yake inaelekea mauti,
Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.
19Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja,[#Mhu 7:26; Ebr 13:4]
Wala hawazifikilii njia za uzima.
20Ili upate kwenda katika njia ya watu wema,[#Ebr 6:12]
Na kuyashika mapito ya wenye haki.
21Maana wanyofu watakaa katika nchi,
Na wakamilifu watadumu ndani yake.
22Bali waovu watatengwa na nchi,
Nao wafanyao hila watang’olewa.