The chat will start when you send the first message.
1Hizi nazo ni mithali za Sulemani, ambazo watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda, walizinakili.
2Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo;[#Rum 11:33; Ayu 29:16]
Bali ni utukufu wa mfalme kuchunguza jambo.
3Mbingu huenda juu sana, na nchi huenda chini;
Lakini mioyo ya wafalme haichunguziki.
4Ondoa takataka katika fedha,
Na chombo kitatokea kwa mtakasaji;
5Mwondoe asiye haki mbele ya mfalme,
Na kiti chake cha enzi kitathibitika katika haki.
6Usijitukuze mbele ya uso wa mfalme;[#Lk 14:8-10]
Wala usisimame mahali pa watu wakuu;
7Kwa maana ni heri kuambiwa, Njoo huku mbele;
Kuliko kuwekwa nyuma machoni pa mkuu.
Yale uliyoyaona kwa macho,
8Usitoke nje kwa haraka ili kuyashindania;[#Mt 5:25]
Usije ukakosa kujua la kutenda hatimaye,
Mwenzako atakapokuwa amekuaibisha.
9Ujitetee na mwenzako peke yake;[#Mt 18:15]
Bali usiifunue siri ya mtu mwingine;
10Yeye asikiaye asije akakutukana;
Na aibu yako isiondoke.
11Neno linenwalo wakati wa kufaa,
Ni kama machungwa katika vyano vya fedha.
12Kipuli cha dhahabu, na pambo la dhahabu safi;
Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo.
13Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno;
Ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwao wamtumao;
Kwa maana huwaburudisha bwana zake nafsi zao.
14Kama mawingu na upepo pasipo mvua;[#Yud 1:12]
Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo.
15Kwa uvumilivu mwingi mkuu husadikishwa;
Na ulimi laini huvunja mfupa.
16Je! Umeona asali? Kula kadiri ya kukutosha;
Usije ukashiba na kuitapika.
17Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi;
Asije akakukinai na kukuchukia.
18Mtu amshuhudiaye jirani yake uongo[#Zab 140:3]
Ni nyundo, na upanga, na mshale mkali.
19Kumtumaini asiye mwaminifu wakati wa taabu[#Ayu 6:14-20; 2 Tim 4:16]
Ni kama jino lililovunjika, au mguu ulioteguka.
20Amwimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito,[#Dan 6:18]
Ni kama yeye avuaye nguo wakati wa baridi;
Ni kama siki juu ya magadi.
21Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula;[#Rum 12:20; Mt 5:44]
Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa;
22Maana utatia makaa ya moto kichwani pake;[#2 Sam 16:12]
Na BWANA atakupa thawabu.
23Upepo wa kusi huleta mvua;
Vile vile asingiziaye huleta uso wa ghadhabu.
24Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini,
Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.
25Kama vile maji ya baridi kwa mtu mwenye kiu,
Ndivyo ilivyo habari njema itokayo katika nchi ya mbali.
26Mwenye haki amwangukiapo mtu mbaya[#Mik 7:8]
Ni kama chemchemi iliyochafuka,
Na kisima kilichokanyagwa.
27Haifai kula asali nyingi mno;[#Lk 14:11]
Vile vile mtu kutafuta utukufu wake mwenyewe si utukufu.
28Asiyetawala roho yake
Ni mfano wa mji uliobomolewa, usio na kuta.