Mit 28

Mit 28

1Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu;

Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.

2Kwa sababu ya maasi ya nchi wakuu wake huwa wengi;

Bali kwa wenye ufahamu na maarifa hali ya nchi hudumishwa

3Mtu mhitaji awaoneaye maskini,[#Mt 18:28]

Ni kama mvua ya dhoruba isiyosaza chakula.

4Wao waiachao sheria huwasifu waovu;[#1 Fal 18:18; Mt 3:7; Efe 5:11; 1 Tim 5:20]

Bali wao waishikao hushindana nao.

5Watu wabaya hawaelewi na hukumu;[#Yn 7:17]

Bali wamtafutao BWANA huelewa na yote.

6Afadhali maskini aendaye katika unyofu wake,

Kuliko mpotofu wa njia angawa ni tajiri.

7Yeye aishikaye sheria ni mwana mwenye hekima;

Bali aliye rafiki wa walafi humwaibisha babaye.

8Yeye azidishaye mali yake kwa riba na faida,

Humkusanyia mtu awahurumiaye maskini.

9Yeye aligeuzaye sikio lake asiisikie sheria,[#2 Tim 4:3; Zab 66:18; Lk 13:25-27]

Hata sala yake ni chukizo.

10Kila mtu awapotezaye wenye haki katika njia mbaya,[#Zab 34:9,10; Mt 6:33; Mk 10:30; Lk 18:29,30; Rum 8:32; 1 Kor 3:22,23]

Ataanguka katika rima lake mwenyewe;

Bali wakamilifu watarithi mema.

11Mtu tajiri ana hekima machoni pake mwenyewe;

Bali maskini mwenye ufahamu humchunguza sana.

12Wenye haki washindapo, uko utukufu mwingi;

Bali waovu waondokapo, watu hujificha.

13Afichaye dhambi zake hatafanikiwa;

Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.

14Mwanadamu mwenye kicho yu heri sikuzote;

Bali mshupavu wa moyo ataangukia madhara.

15Kama simba angurumaye, na dubu mwenye njaa;[#Mt 2:16]

Ndivyo alivyo mtu mbaya awatawalaye maskini.

16Mkuu aliyepungukiwa na akili huwaonea watu sana;

Bali achukiaye kutamani ataongeza siku zake.

17Aliyelemewa na damu ya mtu

Atalikimbilia shimo; wala mtu asimzuie.

18Aendaye kwa unyofu ataokolewa;

Bali mkaidi wa njia zake ataanguka mara.

19Alimaye shamba lake atakuwa na chakula tele;

Bali afuataye mambo ya upuzi atapata umaskini wa kumtosha.

20Mtu mwaminifu atakuwa na baraka tele;

Lakini afanyaye haraka kuwa tajiri hakosi ataadhibiwa.

21Kupendelea watu si kwema;[#Eze 13:19]

Wala mtu kuasi kwa ajili ya kipande cha mkate.

22Mwenye husuda afanya haraka kuwa tajiri;

Wala haufikiri uhitaji utakaomjilia.

23Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali;

Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake.

24Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa;

Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu.

25Mwenye nafsi ya kutamani huchochea fitina;[#1 Tim 6:6]

Bali amtumainiye BWANA atawandishwa.

26Mwenye kujitumainia moyo wake ni mjinga;

Bali yeye aendaye kwa busara ataokolewa.

27Mwenye kuwagawia maskini hatahitaji kitu;

Bali afichaye macho yake atakuwa na laana nyingi.

28Wasio haki wainukapo, wanadamu hujificha;

Bali waangamiapo, wenye haki huongezeka.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania