The chat will start when you send the first message.
1Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo,
Atavunjika ghafula, wala hapati dawa.
2Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi;
Bali mwovu atawalapo, watu huugua.
3Apendaye hekima humfurahisha babaye;[#1 Fal 1:48; Flp 2:22; Mit 10:1; 15:20]
Bali ashikamanaye na makahaba hutapanya mali.
4Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu;
Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.
5Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake,
Hutandika wavu ili kuitega miguu yake.
6Kuna mtego katika kosa la mtu mbaya;
Bali mwenye haki huimba na kufurahi.
7Mwenye haki huyaangalia madai ya maskini;[#Ayu 29:16; Zab 31:7; Isa 35:3,4; Lk 22:32; Gal 6:1]
Bali mtu mbaya hana ufahamu hata ayajue.
8Watu wenye dharau huwasha mji moto;
Bali wenye hekima hugeuzia mbali ghadhabu.
9Mwenye hekima akijadiliana na mpumbavu;
Akikasirika au akicheka, pia hapana raha.
10Wamwagao damu humchukia mtu mkamilifu;
Bali wenye haki humtunza nafsi yake.
11Mpumbavu hudhihirisha hasira yake yote;
Bali mwenye hekima huizuia na kuituliza.
12Mwenye kutawala akisikiliza uongo;
Basi watumishi wake wote watakuwa waovu.
13Maskini na mdhalimu hukutana pamoja;[#Mt 5:45]
BWANA huwatia nuru macho yao wote wawili.
14Mfalme awahukumuye maskini kwa uaminifu;[#Zab 72:2]
Kiti chake cha enzi kitathibitika milele.
15Fimbo na maonyo hutia hekima;
Bali mwana aliyeachiliwa humwaibisha mamaye.
16Waovu wakiongezeka, maasi huongezeka;[#Zab 37:36]
Bali wenye haki watayatazama maanguko yao.
17Mrudi mwanao naye atakustarehesha;[#Mit 13:24]
Naam, atakufurahisha nafsi yako.
18Pasipo maono, watu huacha kujizuia;[#1 Sam 3:1; Amo 8:11; Yn 13:17; Yak 1:25]
Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.
19Haitoshi mtumwa kuonywa kwa maneno;
Maana ajapoyafahamu hataitika.
20Je! Umemwona mtu mwenye kuhamaki katika maneno?
Afadhali kumtumaini mpumbavu kuliko yeye.
21Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto,
Mwisho wake atakuwa ni mwanawe.
22Mtu wa hasira huchochea ugomvi;
Na mtu mwenye ghadhabu huasi sana.
23Kiburi cha mtu kitamshusha;[#Isa 2:11,12; Mt 23:12; Lk 14:11]
Bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa.
24Mshiriki wa mwivi huichukia nafsi yake mwenyewe;[#Law 5:1]
Asikia maapizo, wala hana neno.
25Kuwaogopa wanadamu huleta mtego;[#Mwa 12:12]
Bali amtumainiye BWANA atakuwa salama.
26Watu wengi hutafuta upendeleo wa mkuu;
Bali hukumu ya kila mtu hutoka kwa BWANA
27Mtu aliye dhalimu ni chukizo kwa wenye haki;
Na mnyofu wa mwenendo ni chukizo kwa waovu.