Mit 30

Mit 30

Maneno ya Aguri yenye Hekima

1Maneno ya Aguri bin Yake; mausia mtu huyu aliyomwambia Ithieli, naam, Ithieli na Ukali.

2Hakika nimekuwa kama mnyama, wala si mtu;[#Zab 73:22]

Wala sina ufahamu wa mwanadamu;

3Wala sikujifunza hekima;

Wala sina maarifa ya kumjua Mtakatifu.

4Ni nani aliyepanda mbinguni na kushuka chini?[#Yn 3:13; Ayu 38:4]

Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake?

Ni nani aliyeyafunga maji ndani ya nguo yake?

Ni nani aliyefanya imara ncha zote za nchi?

Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua?

5Kila neno la Mungu limehakikishwa;[#Zab 12:6; 18:30; 84:11]

Yeye ni ngao yao wamwaminio.

6Usiongeze neno katika maneno yake;[#Kum 4:2; Ufu 22:18]

Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.

7Mambo haya mawili nimekuomba;

Usininyime [matatu] kabla sijafa.

8Uniondolee ubatili na uongo;[#Mt 6:11]

Usinipe umaskini wala utajiri;

Unilishe chakula kilicho kadiri yangu.

9Nisije nikashiba nikakukana,[#Kum 8:12; Neh 9:25; Hos 13:6]

Nikasema, BWANA ni nani?

Wala nisiwe maskini sana nikaiba,

Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.

10Usimchongee mtumwa kwa bwana wake;

Asije akakulaani, ukaonekana una hatia.

11Kuna kizazi cha watu wamlaanio baba yao;

Wala hawambariki mama yao.

12Kuna kizazi cha watu walio safi machoni pao wenyewe;[#Isa 65:5; Lk 18:11; Tit 1:15,16]

Ambao hawakuoshwa uchafu wao.

13Kuna kizazi cha watu ambao macho yao yameinuka kama nini!

Na kope zao zimeinuka sana.

14Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga;[#Ayu 29:17; Zab 14:4; Amo 8:4]

Na vigego vyao ni kama visu.

Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu.

15Mruba anao binti wawili,

Waliao, Nipe! Nipe!

Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe,

Naam, vinne visivyosema, Basi!

16Kuzimu; na tumbo lisilozaa;[#Mit 27:20; Hab 2:5]

Nchi isiyoshiba maji; na moto usiosema, Basi!

17Jicho la mtu amdhihakiye babaye,[#Mwa 9:22; Law 20:9]

Na kudharau kumtii mamaye;

Kunguru wa bondeni wataling’oa,

Na vifaranga vya tai watalila.

18Kuna mambo matatu yaliyo ya ajabu kwangu,

Naam, kuna manne nisiyoyafahamu.

19Mwendo wa tai katika hewa;

Na mwendo wa nyoka juu ya mwamba;

Mwendo wa merikebu katikati ya bahari;

Na mwendo wa mtu pamoja na msichana.

20Hivyo ndivyo mwendo wa mwanamke mzinifu;

Hula, akapangusa kinywa chake,

Akasema, Sikufanya uovu.

21Kwa ajili ya mambo matatu nchi hutetemeka,

Naam, kwa ajili ya manne haiwezi kuvumilia.

22Mtumwa apatapo kuwa mfalme;[#Mit 19:10; Mhu 10:7]

Mpumbavu ashibapo chakula;

23Mwanamke mwenye kuchukiza aolewapo;

Na mjakazi aliye mrithi wa bibi yake.

24Kuna viumbe vinne duniani vilivyo vidogo;

Lakini vina akili nyingi sana.

25Chungu ni watu wasio na nguvu;[#Mit 6:6]

Lakini hujiwekea chakula wakati wa hari.

26Wibari ni watu dhaifu;[#Law 11:5; Zab 104:18]

Lakini hujifanyia nyumba katika miamba.

27Nzige hawana mfalme;

Lakini huenda wote pamoja vikosi vikosi.

28Mjusi hushika kwa mikono yake;

Lakini yumo majumbani mwa wafalme.

29Kuna watatu wenye mwendo wa kupendeza,

Naam, wanne walio na mwendo mzuri.

30Simba aliye hodari kupita wanyama wote;

Wala hajiepushi na aliye yote;

31Jimbi aendaye tambo; na beberu;

Na mfalme ambaye haasiki.

32Ikiwa umefanya kipumbavu kwa kujikuza;[#Mhu 8:3; Mik 7:16; Rum 3:19]

Au ikiwa umewaza mabaya;

Basi weka mkono wako juu ya kinywa chako.

33Kwa maana kupiga maziwa huleta siagi;

Na kupiga pua hutokeza damu;

kadhalika kuchochea hasira hutokeza ugomvi.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania