Zab 102

Zab 102

Sala ya Kutaka Msaada kutoka kwa Mungu

1Ee BWANA, usikie kuomba kwangu,

Kilio changu kikufikie.

2Usinifiche uso wako siku ya shida yangu,

Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.

3Maana siku zangu zinatoweka kama moshi,[#Yak 4:14; Omb 1:13]

Na mifupa yangu inateketea kama kinga.

4Moyo wangu umepigwa kama majani na kukauka,

Naam, ninasahau kula chakula changu.

5Kwa ajili ya sauti ya kuugua kwangu

Mifupa yangu imegandamana na nyama yangu.

6Nimekuwa kama mwari nyuni wa jangwani,[#Isa 34:11; Sef 2:14]

Na kufanana na bundi wa mahameni.

7Nakesha, tena nimekuwa kama shomoro

Aliye peke yake juu ya nyumba.

8Adui zangu wananilaumu mchana kutwa;[#Mdo 23:12]

Wanaonichukia kana kwamba wana wazimu

Huapa kwa kunitaja mimi.

9Maana nimekula majivu kama chakula,

Na kukichanganya kinywaji changu na machozi.

10Kwa sababu ya ghadhabu yako na hasira yako;[#Zab 30:7]

Maana umeniinua na kunitupilia mbali.

11Siku zangu zi kama kivuli kilichotandaa,[#Yak 1:10]

Nami ninanyauka kama majani.

12Bali Wewe, BWANA utaketi ukimiliki milele,[#1 Tim 6:16]

Na kumbukumbu lako kizazi hata kizazi.

13Wewe mwenyewe utasimama,[#Isa 40:2]

Na kuirehemu Sayuni,

Kwa maana ndio wakati wa kuihurumia,

Naam, majira yaliyoamriwa yamewadia.

14Maana watumishi wako wameyaridhia mawe yake,[#Dan 9:2]

Na kuyaonea huruma mavumbi yake.

15Kisha mataifa wataliogopa jina la BWANA,[#1 Fal 8:43]

Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;

16BWANA atakapokuwa ameijenga Sayuni,

Atakapoonekana katika utukufu wake,

17Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,[#Neh 2:8]

Asiyadharau maombi yao.

18Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,[#Rum 15:4; 1 Kor 10:11; Zab 22:31; Isa 43:21]

Na watu watakaoumbwa watamsifu BWANA.

19Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,[#Kum 26:15; Zab 14:2]

Toka mbinguni BWANA ameiangalia nchi,

20Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,

Na kuwafungua walioandikiwa kufa.

21Watu walitangaze jina la BWANA katika Sayuni,

Na sifa zake katika Yerusalemu,

22Pindi mataifa watapokusanyika pamoja,[#Hos 1:11]

Falme nazo ili kumtumikia BWANA.

23Amezipunguza nguvu zangu njiani;

Amezifupisha siku zangu.

24Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu;[#Zab 90:2; Hab 1:12; Ufu 1:4,8]

Miaka yako ni tangu kizazi hata kizazi.

25Hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi,[#Mwa 1:1; Kut 20:11; Ayu 38:4-7; Ebr 1:10-12]

Na mbingu ni kazi ya mikono yako.

26Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu[#Isa 66:22; Rum 8:20; 2 Pet 3:7]

Naam, hizi zitachakaa kama nguo;

Na kama mavazi utazibadilisha,

Nazo zitabadilika.

27Lakini Wewe U Yeye yule;[#Mal 3:6]

Na miaka yako haitakoma.

28Wana wa watumishi wako watakaa,

Na wazao wao wataimarishwa mbele zako.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania