Zab 105

Zab 105

Uaminifu wa Mungu kwa Israeli

1Haleluya.[#Isa 12:4; #105:1 maana yake ni, Msifuni BWANA.]

Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake,

Wajulisheni watu matendo yake.

2Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi,

Zitafakarini ajabu zake zote.

3Jisifuni kwa jina lake takatifu,

Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA.

4Mtakeni BWANA na nguvu zake,[#Zab 27:8]

Utafuteni uso wake sikuzote.

5Zikumbukeni ajabu zake alizozifanya,[#Kum 8:2]

Miujiza yake na hukumu za kinywa chake.

6Enyi wazao wa Ibrahimu, mtumishi wake;

Enyi wana wa Yakobo, wateule wake.

7Yeye, BWANA, ndiye Mungu wetu;[#Isa 26:9]

Duniani mwote mna hukumu zake.

8Analikumbuka agano lake milele;[#Lk 1:72]

Neno lile aliloviamuru vizazi elfu.

9Agano alilofanya na Ibrahimu,[#Mwa 12:7; 17:8; 26:3; #Mwa 17:2; 22; 16; 26:3; Zab 111:5,9; Dan 9:4; Lk 1:73; Ebr 6:17]

Na uapo wake kwa Isaka.

10Alilomthibitishia Yakobo liwe amri,[#Mwa 28:13]

Na Israeli liwe agano la milele.

11Akisema, Nitakupa wewe nchi ya Kanaani,[#Mwa 15:18]

Iwe urithi wenu mliopimiwa.

12Walipokuwa watu wawezao kuhesabiwa,[#Mwa 34:30; Kum 7:7; Mwa 17:8; Ebr 11:9]

Naam, watu wachache na wageni ndani yake,

13Wakatanga-tanga toka taifa hata taifa,

Toka ufalme mmoja hata kwa watu wengine.

14Hakumwacha mtu awaonee,[#Mwa 12:17; 20:3-7; 35:5]

Hata wafalme aliwakemea kwa ajili yao.

15Akisema, Msiwaguse masihi wangu,[#105:15 Au, mtiwa mafuta.]

Wala msiwadhuru nabii zangu.

16Akaiita njaa iijilie nchi,[#Mwa 41:53-57; 2 Fal 8:1; Law 26:26]

Akakiharibu chakula chote walichokitegemea.

17Alimpeleka mtu mbele yao,[#Mwa 37:28; 45:5]

Yusufu aliuzwa utumwani.

18Walimwumiza miguu yake kwa pingu,[#Mwa 39:20—40:15,23]

Akatiwa katika minyororo ya chuma.

19Hata wakati wa kuwadia neno lake,

Ahadi ya BWANA ilimjaribu.

20Mfalme alituma watu akamfungua,[#Mwa 41:14]

Mkuu wa watu akamwachia.

21Akamweka kuwa bwana wa nyumba yake,[#Mwa 41:39-41]

Na mwenye amri juu ya mali zake zote.

22Awafunge masheki wake kama apendavyo,

Na kuwafundisha wazee wake hekima.

23Israeli naye akaingia Misri,[#Mwa 46:6; 47:11]

Yakobo akawa mgeni katika nchi ya Hamu.

24Akawajalia watu wake wazae sana,[#Kut 1:7-14; Kum 26:5; Mdo 7:17]

Akawafanya kuwa hodari kuliko watesi wao.

25Akawageuza moyo wawachukie watu wake,

Wakawatendea hila watumishi wake.

26Akamtuma Musa, mtumishi wake,[#Kut 3:10—4:17; Hes 16:5]

Na Haruni ambaye amemchagua.

27Akaweka mambo ya ishara zake kati yao,

Na miujiza katika nchi ya Hamu.

28Alituma giza, kukafunga giza,[#Kut 10:21-23; Zab 99:7]

Wala hawakuyaasi maneno yake.

29Aliyageuza maji yao yakawa damu,[#Kut 7:17-21]

Akawafisha samaki wao.

30Nchi yao ilijaa vyura,[#Kut 8:1-6]

Vyumbani mwa wafalme wao.

31Alisema, kukaja makundi ya mainzi,[#Kut 8:16-17,20-24]

Na chawa mipakani mwao mwote.

32Badala ya mvua aliwapa mvua ya mawe,[#Kut 9:22-25]

Na moto wa miali katika nchi yao.

33Akaipiga mizabibu yao na mitini yao,

Akaivunja miti ya mipaka yao.

34Alisema, kukaja nzige,[#Kut 10:12-15]

Na tunutu wasiohesabika;

35Wakaila miche yote ya nchi yao,

Wakayala matunda ya ardhi yao.

36Akawapiga wazaliwa wa kwanza katika nchi,[#Mwa 49:3; Kut 12:29]

Malimbuko ya nguvu zao.

37Akawatoa hali wana fedha na dhahabu,[#Kut 12:33-36]

Katika kabila zao asiwepo mwenye kukwaa.

38Misri ilifurahi walipoondoka,

Maana kwa ajili yao hofu imewaangukia.

39Alitandaza wingu liwe funiko,[#Kut 13:21-22; Neh 9:12]

Na moto utoe nuru usiku.

40Walipotaka akaleta kware,[#Kut 16:2-15]

Akawashibisha chakula cha mbinguni.

41Akaufunua mwamba, kukabubujika maji,[#Kut 17:1-7; Hes 20:2-13; Neh 9:15; Isa 48:21; 1 Kor 10:4]

Yakapita pakavuni kama mto.

42Maana alilikumbuka neno lake takatifu,

Na Ibrahimu, mtumishi wake.

43Akawatoa watu wake kwa shangwe,

Na wateule wake kwa nyimbo za furaha.

44Akawapa nchi za mataifa, wakairithi kazi ya watu;[#Kum 6:10; Yos 11:16-23; 13:7]

45Ili wazishike amri zake, na kuzitii sheria zake.[#Kum 4:1]

Haleluya.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania