The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu wa sifa zangu, usinyamaze,[#Zab 83:1]
2Kwa maana wamenifumbulia kinywa;
Kinywa cha mtu asiye haki, cha hila,
Wamesema nami kwa ulimi wa uongo.
3Naam, kwa maneno ya chuki wamenizunguka,[#1 Sam 19:4,5; Zab 35:7,20; Yn 15:25]
Wamepigana nami bure.
4Badala ya upendo wangu wao hunishitaki,
Ijapokuwa naliwaombea.
5Wamenichukuza mabaya badala ya mema,[#Zab 38:20]
Na chuki badala ya upendo wangu.
6Uweke mtu mkorofi juu yake,
Mshitaki asimame mkono wake wa kuume.
7Katika kuhukumiwa ataonekana hana haki,[#Mit 28:9]
Na sala yake itadhaniwa kuwa ni dhambi.
8Siku zake na ziwe chache,[#Mdo 1:20]
Usimamizi wake na atwae mtu mwingine.
9Wanawe na wawe yatima,[#Kut 22:24; Yer 18:21]
Na mkewe na awe mjane.
10Kutanga na watange wanawe na kuomba,[#Mwa 4:12]
Watafute chakula mbali na mahame yao.
11Mdai na anase vitu vyote alivyo navyo,[#Ayu 18:9]
Wageni na wateke mapato ya kazi yake.
12Asiwe na mtu wa kumfanyia fadhili,
Wala mtu wa kuwahurumia yatima wake.
13Wazao wake waangamizwe,[#Zab 37:28; Mit 10:7]
Jina lao likafutwe katika kizazi cha pili.
14Uovu wa baba zake ukumbukwe mbele za BWANA,[#Kut 20:5; Neh 4:5]
Na dhambi ya mamaye isifutwe.
15Ziwe mbele za BWANA daima,[#Ayu 18:17]
Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
16Kwa kuwa hakukumbuka kutenda fadhili,
Bali alimfukuza mnyonge na mhitaji,
Hata akamfisha mtu aliyevunjika moyo,
17Naye alipenda kulaani, nako kukampata.
Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye,
18Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake.
Ikamwingilia moyoni kama maji,
Na kama mafuta mifupani mwake.
19Na iwe kwake kama vazi ajivikalo,
Na kama mshipi ajifungao daima.
20Ndiyo malipo ya washitaki wangu toka kwa BWANA,
Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu mabaya.
21Na Wewe, MUNGU, Bwana, unitendee kwa ajili ya jina lako,
Kwa kuwa fadhili zako ni njema uniokoe.
22Kwa maana mimi ni mnyonge na mhitaji,
Na moyo wangu umejeruhi ndani yangu.
23Ninapita kama kivuli kianzacho kutoweka,
Ninapeperushwa kama nzige.
24Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga,[#Ebr 12:12]
Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta.
25Nami nalikuwa laumu kwao,[#Isa 37:22; Mt 27:39; Mk 15:29]
Wanionapo hutikisa vichwa vyao.
26Ee BWANA, Mungu wangu, unisaidie,
Uniokoe sawasawa na fadhili zako.
27Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako;[#Ayu 37:7]
Wewe, BWANA, umeyafanya hayo.
28Wao walaani, bali Wewe utabariki,[#Hes 22:12; Isa 65:14]
Wameondoka wao wakaaibishwa,
Bali mtumishi wako atafurahi.
29Washitaki wangu watavikwa fedheha,
Watajivika aibu yao kama joho.
30Nitamshukuru BWANA kwa kinywa changu,
Naam, nitamsifu katikati ya mkutano.
31Maana atasimama mkono wa kuume wa mhitaji
Amwokoe na wanaoihukumu nafsi yake.