Zab 141

Zab 141

Sala ya Kutaka Kulindwa kutoka kwa Uovu

1Ee BWANA, nimekuita, unijie hima,

Uisikie sauti yangu nikuitapo.

2Sala yangu ipae mbele zako kama uvumba,[#Efe 5:2; 1 Tim 2:8; Ufu 5:8]

Kuinuliwa mikono yangu kama dhabihu ya jioni.

3Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu,

Mngojezi mlangoni pa midomo yangu.

4Usiuelekeze moyo wangu kunako jambo baya,[#Mt 6:14; 20:15; Mit 23:6]

Nisiyazoelee matendo yasiyofaa,

Pamoja na watu watendao maovu;

Wala nisile vyakula vyao vya anasa.

5Mwenye haki na anipige, itakuwa fadhili;

Anikemee, itakuwa kama mafuta kichwani;

Kichwa changu kisikatae,

Maana siachi kusali kati ya mabaya yao.

6Makadhi wao wakiangushwa kando ya genge,

Watayasikia maneno yangu, maana ni matamu.

7Kama kupasua kuni na kuzichanja juu ya nchi,[#2 Kor 1:9]

Ndivyo ilivyo mifupa yetu mdomoni pa kuzimu.

8Macho yangu yanakuelekea Wewe, MUNGU Bwana,[#Zab 25:15]

Nimekukimbilia Wewe, usiniache nafsi yangu.

9Unilinde na mtego walionitegea,

Na matanzi yao watendao maovu.

10Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe,[#Est 7:10; Zab 7:15]

Pindi mimi ninapopita salama.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania