The chat will start when you send the first message.
1Mungu, unihifadhi mimi,[#Zab 25:20]
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
2Nimemwambia BWANA, Ndiwe BWANA wangu;
Sina wema ila utokao kwako.
3Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora,
Hao ndio niliopendezwa nao.
4Huzuni zao zitaongezeka
Wambadilio Mungu kwa mwingine;
Sitazimimina sadaka zao za damu,
Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu.
5BWANA ndiye fungu la posho langu,
Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
6Kamba zangu zimeniangukia mahali pema,
Naam, nimepata urithi mzuri.
7Nitamhimidi BWANA aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
8Nimemweka BWANA mbele yangu daima,[#Mdo 2:25-28]
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
9Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
10Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu,[#Mdo 13:35; Zab 49:15; Mdo 2:27; Dan 9:24; Lk 1:35]
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.
11Utanijulisha njia ya uzima;[#Mdo 2:28]
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume
Mna mema ya milele.