The chat will start when you send the first message.
1Wewe, BWANA, nguvu zangu, nakupenda sana;[#Kum 32:4; 1 Sam 2:2; Zab 91:2]
2BWANA ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu,[#Ebr 2:13]
Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia,
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
3Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa,[#Zab 76:4]
Hivyo nitaokoka na adui zangu.
4Kamba za mauti zilinizunguka,[#Zab 116:3]
Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
5Kamba za kuzimu zilinizunguka,
Mitego ya mauti ikanikabili.
6Katika shida yangu nalimwita BWANA,
Na kumlalamikia Mungu wangu.
Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,
Kilio changu kikaingia masikioni mwake.
7Ndipo nchi iliyotikisika na kutetemeka,[#Mdo 4:31]
Misingi ya milima ikasuka-suka;
Ikatikisika kwa sababu alikuwa na ghadhabu.
8Kukapanda moshi kutoka puani mwake,
Moto ukatoka kinywani mwake ukala,
Makaa yakawashwa nao.
9Aliziinamisha mbingu akashuka,[#Isa 64:1]
Kukawa na giza kuu chini ya miguu yake.
10Akapanda juu ya kerubi akaruka,[#Zab 99:1; 104:3]
Naam, aliruka upesi juu ya mabawa ya upepo.
11Alifanya giza kuwa mahali pake pa kujificha,[#Zab 97:2]
Kuwa hema yake ya kumzunguka.
Giza la maji na mawingu makuu ya mbinguni.
12Toka mwangaza uliokuwa mbele zake
Kukapita mawingu yake makuu.
Mvua ya mawe na makaa ya moto.
13BWANA alipiga radi mbinguni,[#Zab 29:3]
Yeye Aliye juu akaitoa sauti yake,
Mvua ya mawe na makaa ya moto.
14Akaipiga mishale yake akawatawanya,[#Hes 24:8; Kum 32:23; Ayu 6:4; Zab 21:12]
Naam, umeme mwingi sana, akawatapanya.
15Ndipo ilipoonekana mikondo ya maji,
Misingi ya ulimwengu ikafichuliwa,
Ee BWANA, kwa kukemea kwako,
Kwa mvumo wa pumzi ya puani mwako.
16Alipeleka kutoka juu akanishika,[#Zab 144:7]
Na kunitoa katika maji mengi.
17Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu,
Na wale walionichukia,
Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi.
18Walinikabili siku ya msiba wangu,
Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu.
19Akanitoa akanipeleka panapo nafasi,[#Zab 118:5]
Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami.
20BWANA alinitendea sawasawa na haki yangu,[#2 Sam 22:21; Mit 18:10; Mt 6:4; 1 Kor 3:8]
Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa.
21Maana nimezishika njia za BWANA,
Wala sikumwasi Mungu wangu.
22Hukumu zake zote zilikuwa mbele yangu,
Wala amri zake sikujiepusha nazo.
23Nami nalikuwa mkamilifu mbele zake,
Nikajilinda na uovu wangu.
24Mradi BWANA amenilipa sawasawa na haki yangu,[#Rut 2:12; Mt 10:41,42]
Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.
25Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili;[#Mt 18:32-35]
Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;
26Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu;[#Law 26:23]
Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi.
27Maana Wewe utawaokoa watu wanaoonewa,[#Mit 6:17]
Na macho ya kiburi utayadhili.
28Kwa kuwa Wewe unaiwasha taa yangu;[#Ayu 18:6]
BWANA Mungu wangu aniangazia giza langu.
29Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi,
Kwa msaada wa Mungu wangu naruka ukuta.
30Mungu, njia yake ni kamilifu,[#Kum 32:4; Rum 12:3; Ufu 15:3; Zab 12:6]
Ahadi ya BWANA imehakikishwa,
Yeye ndiye ngao yao.
Wote wanaomkimbilia.
31Maana ni nani aliye Mungu ila BWANA?[#Kum 32:31; 2 Sam 22:32]
Ni nani aliye mwamba ila Mungu wetu?
32Mungu ndiye anifungaye mshipi wa nguvu,
Naye anaifanya kamilifu njia yangu.
33Miguu yangu anaifanya kuwa ya kulungu,[#Hab 3:19]
Na kunisimamisha mahali pangu pa juu.
34Ananifundisha mikono yangu vita,
Mikono yangu ikaupinda upinde wa shaba.
35Nawe umenipa ngao ya wokovu wako,
Mkono wako wa kuume umenitegemeza,
Na unyenyekevu wako umenikuza.
36Umezifanyizia nafasi hatua zangu,
Na miguu yangu haikuteleza.
37Nitawafuatia adui zangu na kuwapata,
Wala sitarudi nyuma hata wakomeshwe.
38Nitawapiga-piga wasiweze kusimama,
Wataanguka chini ya miguu yangu.
39Nawe hunifunga mshipi wa nguvu kwa vita,
Hunitiishia chini yangu walioniondokea.
40Naam, adui zangu umewafanya wanipe visogo,
Nao walionichukia nimewakatilia mbali.
41Walipiga yowe, lakini hakuna wa kuokoa,[#Mit 1:28]
Walimwita BWANA lakini hakuwajibu,
42Nikawaponda kama mavumbi mbele ya upepo,
Nikawatupa nje kama matope ya njiani.
43Umeniokoa na mashindano ya watu,
Umenifanya niwe kichwa cha mataifa.
Watu nisiowajua walinitumikia.
44Kwa kusikia tu habari zangu,
Mara wakanitii.
Wageni walinijia wakinyenyekea.
45Wageni nao walitepetea,[#Mik 7:17]
Walitoka katika ngome zao wakitetemeka.
46BWANA ndiye aliye hai;[#Yer 10:10]
Na ahimidiwe mwamba wangu;
Na atukuzwe Mungu wa wokovu wangu;
47Ndiye Mungu anipatiaye kisasi;
Na kuwatiisha watu chini yangu.
48Huniponya na adui zangu;[#Zab 59:1]
Naam, waniinua juu yao walioniinukia,
Na kuniponya na mtu wa jeuri.
49Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa,[#Rum 15:9]
Nami nitaliimbia jina lako.
50Ampa mfalme wake wokovu mkuu,[#Zab 144:10]
Amfanyia fadhili masihi wake,
Daudi na mzao wake hata milele.