The chat will start when you send the first message.
1Ee BWANA, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
2Ee BWANA, Mungu wangu,[#Zab 6:2-4]
Nalikulilia ukaniponya.
3Umeniinua nafsi yangu,[#Zab 40:1,2]
Ee BWANA, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni.
4Mwimbieni BWANA zaburi,
Enyi watauwa wake.
Na kufanya shukrani.
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
5Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,[#Zab 16:11; Ufu 22:17]
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha.
6Nami nilipofanikiwa nalisema,[#Ayu 29:18]
Sitaondoshwa milele.
7BWANA, kwa radhi yako[#Zab 104:29]
Wewe uliuimarisha mlima wangu.
Uliuficha uso wako,
Nami nikafadhaika.
8Ee BWANA, nalikulilia Wewe,
Naam, kwa BWANA naliomba dua.
9Mna faida gani katika damu yangu[#Zab 115:17]
Nishukapo shimoni?
Mavumbi yatakusifu?
Yataitangaza kweli yako?
10Ee BWANA, usikie, unirehemu,[#Zab 4:1]
BWANA, uwe msaidizi wangu.
11Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;[#2 Sam 6:14]
Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
12Ili utukufu wangu ukusifu,
Wala usinyamaze.
Ee BWANA, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele.