Zab 39

Zab 39

Sala ya Kutaka Hekima na Msamaha

1Nalisema, Nitazitunza njia zangu[#1 Fal 2:4; Mit 4:26,27; Ebr 2:1; Kol 4:5]

Nisije nikakosa kwa ulimi wangu;

Nitajitia lijamu kinywani,

Maadamu mtu mbaya yupo mbele yangu.

2Nalikuwa sisemi, nalinyamaa kimya,

Sina faraja, maumivu yangu yakazidi.

3Moyo wangu ukawa moto ndani yangu,[#Yer 20:9]

Na katika kuwaza kwangu moto ukawaka;

Nalisema kwa ulimi wangu,

4BWANA, unijulishe mwisho wangu,

Na kiasi cha siku zangu ni kiasi gani;

Nijue jinsi nilivyo dhaifu.

5Tazama, umefanya siku zangu kuwa mashubiri;[#Zab 90:4]

Maisha yangu ni kama si kitu mbele zako.

Kila mwanadamu, ingawa amesitawi, ni ubatili.

6Binadamu huenda tu huko na huko kama kivuli;

Hufanya ghasia tu kwa ajili ya ubatili;

Huweka akiba wala hajui ni nani atakayeichukua.

7Na sasa ninangoja nini, Ee Bwana?

Matumaini yangu ni kwako.

8Uniokoe na maasi yangu yote,

Usinifanye laumu ya mpumbavu.

9Nimenyamaza, sitafumbua kinywa changu,

Maana Wewe ndiwe uliyeyafanya.

10Uniondolee pigo lako;

Kwa uadui wa mkono wako nimeangamia.

11Ukimrudi mtu kwa kumkemea kwa uovu wake,

Watowesha uzuri wake kama nondo.

Kila mwanadamu ni ubatili.

12Ee BWANA, usikie maombi yangu,[#Law 25:23; 1 Nya 29:15]

Utege sikio lako niliapo,

Usiyanyamalie machozi yangu.

Kwa maana mimi ni mgeni wako,

Msafiri kama baba zangu wote.

13Uniachilie nikunjuke uso,[#Ayu 10:20,21]

Kabla sijaondoka nisiwepo tena.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania