Zab 45

Zab 45

Wimbo wa Arusi ya Kifalme

1Moyo wangu umefurika kwa neno jema,

Mimi nasema niliyomfanyizia mfalme;

Ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi mstadi.

2Wewe u mzuri sana kuliko wanadamu;

Neema imemiminiwa midomoni mwako,

Kwa hiyo Mungu amekubariki hata milele.

3Jifungie upanga wako pajani, wewe uliye hodari,

Utukufu ni wako na fahari ni yako.

4Katika fahari yako usitawi uendelee

Kwa ajili ya kweli na upole na haki

Na mkono wako wa kuume

Utakufundisha mambo ya kutisha.

5Mishale yako ni mikali, watu huanguka chini yako;

Imo mioyoni mwa adui za mfalme.

6Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha milele na milele,[#Ebr 1:8-9; Zab 93:2; Isa 9:6,7]

Fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili.

7Umeipenda haki;[#Zab 33:5; Mt 3:15; Ebr 1:9; Isa 61:1; Yn 20:17]

Umeichukia dhuluma.

Kwa hiyo MUNGU, Mungu wako, amekupaka mafuta,

Mafuta ya furaha kuliko wenzako.

8Mavazi yako yote hunukia manemane

Na udi na mdalasini.

Katika majumba ya pembe

Vinubi vimekufurahisha.

9Binti za wafalme wamo

Miongoni mwa akina bibi wako wastahiki.

Mkono wako wa kuume amesimama malkia

Amevaa dhahabu ya Ofiri.

10Sikia, binti, utazame, utege sikio lako,[#Kum 21:13]

Uwasahau watu wako na nyumba ya baba yako.

11Naye mfalme atautamani uzuri wako,[#Zab 95:6; Isa 54:5]

Maana ndiye bwana wako, nawe umsujudie.

12Na binti Tiro analeta kipawa chake,

Nao matajiri wa watu watajipendekeza kwako.

13Binti mfalme yumo ndani ana fahari tupu,[#Ufu 19:7,8]

Mavazi yake ni ya nyuzi za dhahabu.

14Atapelekwa kwa mfalme

Na mavazi yaliyofumwa kwa uzuri.

Wanawali wenzake wanaomfuata,

Watapelekwa kwako.

15Watapelekwa kwa furaha na shangwe,

Na kuingia katika nyumba ya mfalme.

16Badala ya baba zako watakuwapo watoto wako,[#1 Pet 2:9; Ufu 1:6]

Utawafanya kuwa wakuu katika nchi zote.

17Jina lako nitalifanya kuwa kumbukumbu[#Isa 11:10; Mal 1:11]

Katika vizazi vyote.

Kwa hiyo mataifa watakushukuru

Milele na milele.

Swahili Union Version (SUV): © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 1952, 1997. All rights reserved. lt/pgt ltpgtSwahili Union Version (SUV): Hakimiliki -1952, 1997: kwa: Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania