The chat will start when you send the first message.
1Ee Mungu, mpe mfalme hukumu zako,
Na mwana wa mfalme haki yako.
2Atawaamua watu wako kwa haki,[#Isa 11:2]
Na watu wako walioonewa kwa hukumu.
3Milima itawazalia watu amani,
Na vilima navyo kwa haki.
4Atawahukumu walioonewa wa watu,
Atawaokoa wahitaji, atamseta mwenye kuonea.
5Watakuogopa wakati wote wa kudumu jua,
Na wakati wa kung’aa mwezi kizazi hata kizazi.
6Atashuka kama mvua juu ya majani yaliyokatwa,[#2 Sam 23:4; Hos 6:3]
Kama manyunyu yainyweshayo nchi.
7Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi,[#Isa 2:4; Dan 2:44; Lk 1:33]
Na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.
8Na awe na enzi toka bahari hata bahari,[#Kut 23:31; 1 Fal 4:21,24; Zab 2:8; Zek 9:10]
Toka Mto hata miisho ya dunia.
9Wakaao jangwani na wainame mbele zake;
Adui zake na warambe mavumbi.
10Wafalme wa Tarshishi na visiwa na walete kodi;[#Isa 49:7]
Wafalme wa Sheba na Seba na watoe vipawa.
11Naam, wafalme wote na wamsujudie;
Na mataifa yote wamtumikie.
12Kwa maana atamkomboa mhitaji aliapo,
Na mtu aliyeonewa iwapo hana msaidizi.
13Atamhurumia aliye dhaifu na maskini,
Na nafsi za wahitaji ataziokoa.
14Atawakomboa nafsi zao na kuonewa na udhalimu,
Na damu yao ina thamani machoni pake.
15Basi na aishi;[#Mt 6:10; 1 Kor 1:2,3]
Na wampe dhahabu ya Sheba;
Na wamwombee daima;
Na kumbariki mchana kutwa.
16Na uwepo wingi wa nafaka[#1 Fal 4:20]
Katika ardhi juu ya milima;
Matunda yake na yawaye-waye kama Lebanoni,
Na watu wa mjini wasitawi kama majani ya nchi.
17Jina lake na lidumu milele,[#Mwa 12:3; Yer 4:2; Isa 45:23,24; Lk 1:48; Flp 2:9-11]
Pindi ling’aapo jua jina lake liwe na wazao;
Mataifa yote na wajibariki katika yeye,
Na kumwita heri.
18Na ahimidiwe BWANA, Mungu, Mungu wa Israeli,
Atendaye miujiza Yeye peke yake;
19Jina lake tukufu na lihimidiwe milele;
Dunia yote na ijae utukufu wake. Amina na Amina.
20Maombi ya Daudi mwana wa Yese yamekwisha.